Mustafi bora kuliko Van Dijk

Muktasari:

  • Hilo limekuja baada ya beki huyo kuhusika kwenye mabao yote mawili yaliyowafanya Arsenal wapoteze mechi yao dhidi ya Crystal Palace huku mchambuzi na beki wa zamani wa Liverpool, Jamie Carragher akimsema mchezaji huyo kuwa ni janga.

LONDON, ENGLAND.KWELI kila muwamba ngoma anavutia kwake. Kuna shabiki mmoja wa Arsenal ameibuka na kudai kwamba Shkodran Mustafi ni beki bora zaidi kwenye Ligi Kuu England kuliko Virgil van Dijk wa Liverpool kwa msimu huu.

Shabiki huyo ameamua kuibuka na takwimu zake kuonyesha kwamba kile anachokizungumza ni cha kweli kwamba beki wake wa Arsenal ni bora kuliko Van Dijk anayepigiwa debe kuwa ni bora na anapaswa kushindania tuzo ya kuwa mchezaji bora kwenye Ligi Kuu England msimu huu.

Takwimu zake zinaonyesha kwamba Mustafi amefanya tako nyingi na kuwahi mipira njiani mara nyingi huku akiwa amecheza mechi chache kuliko alizocheza staa huyo wa Liverpool. Shabiki huyo ameamua kuja na takwimu hizo baada ya kuona kundi kubwa la mashabiki wenzake kumchoka beki Mustafi na kutaka aondolewe kwenye kikosi mwishoni mwa msimu huu.

Hilo limekuja baada ya beki huyo kuhusika kwenye mabao yote mawili yaliyowafanya Arsenal wapoteze mechi yao dhidi ya Crystal Palace huku mchambuzi na beki wa zamani wa Liverpool, Jamie Carragher akimsema mchezaji huyo kuwa ni janga.

Lakini, shabiki mmoja wa Arsenal akaamua kuja na data zake kumtetea Mustafi na kuonyesha ni beki bora kuliko Van Dijk, ambaye aliigharimu Liverpool Pauni 75 milioni kunasa huduma yake Januari mwaka jana.

Van Dijk katika mechi 35 alizocheza amefanya tako 34 huku akifanikiwa kwa asilimia 71, wakati Mustafi amecheza mechi 28 tu na kupiga tako 55 zikiwa sahihi kwa asilimia 73 huku akiwa amenasa mipira njiani mara 54 dhidi ya 39 za Van Dijk.

Shabiki huyo amedai haoni kitu kinachomfanya Mustafi aonekane si kitu wakati kama ni mabao wote wamefunga idadi sawa kwa kichwa, wakiweka wavuni mara mbili.