Mudathir : Alishusha mjengo kwanza halafu mengine baadaye

Muktasari:

Kiungo huyo amepiga stori na Mwanaspoti na kufunguka mambo mengi iliwa ni sambamba na namna alivyolipokea suala la kutolewa kwa mkopo na kupelekwa Singida United.

HAKUWA tegemeo sana hasa aliposajiliwa kwa mara ya kwanza na Azam FC msimu wa mwaka 2013 akiwa sambamba na kina Aishi Manula akitoka Azam B, lakini Mudathir Yahya sasa ni jembe pale Azam FC.

Awali, maisha ya Mudathir yalikuwa magumu ndani ya Azam na alijikuta akikosa nafasi ya kucheza na kuomba kutolewa kwa mkopo Singida United.

Kutokana na uwezo aliokuwa nao na alikuwa akikubalika zaidi na Hans Van Pluijm haikuwa kazi kupokelewa Singida ambapo aliingia moja kwa moja kikisi cha kwanza.

Kiungo huyo amepiga stori na Mwanaspoti na kufunguka mambo mengi iliwa ni sambamba na namna alivyolipokea suala la kutolewa kwa mkopo na kupelekwa Singida United.

MKOPO ULIMJENGA

Wakati wachezaji wengi wakiamini kutolewa kwa mkopo ni kuua vipaji vyao na wengine wakijikuta wakigomea mchakato huo, kwa Mudathir anathibitisha kuwa yeye kwake kulimpa changamoto ya kupambana zaidi na kuwaonyesha waliomtoa kuwa walikosea.

Mudathir alipelekwa Singida United ambapo alionyesha uwezo wa hali ya juu ambao ulimshawishi aliyekuwa kocha wa timu hiyo, Hans Van Pluijm kumpa kitambaa cha unahodha ili kuwaongoza nyota wenzake uwanjani.

Haitokei mara nyingi kwa mchezaji aliyeko kwa mkopo kufanya kama alivyofanya Mudathir ambaye alicheza kwa uwezo na kuwashawishi viongozi wake wa zamani kumrudisha.

“Kutolewa kwa mkopo kwa mchezaji hakuna maana mchezaji hatakiwi, ameshuka kiwango au hana thamani klabuni japo, wengi wanaamini hivyo mimi sikutaka kuwaaminisha wachezaji wenzangu zaidi nilipambana,” anasema.

PLUIJM ALIMRUDISHA DIMBANI

Soka lina changamoto zake pamoja na sasa kuchukuliwa kama kazi kama zilivyo kazi nyingine, wachezaji wengi wamekuwa wakikumbana na changamoto hizo na kujikuta wanatamani kuachana na kazi hiyo, lengo likiwa ni kuhakikisha wanajitengenezea mazingira ya kuwa huru na majukumu yao.

“Nikiambiwa nitaje watu zaidi ya watatu walionisaidia, basi nakuhakikishia kuwa Hans ni miongoni mwa watu hao kwani ndiye aliyeniaminisha kuwa bado nina nafasi ya kucheza na nikarudi kama ilivyokuwa awali namshukuru Mungu ilikuwa hivyo kweli,” anasema.

“Nakumbuka nikiwa Azam FC nilikuwa sina namba kikosi cha Kocha Aristica Cioaba, ndio Hans alipouomba uongozi wa Azam FC kunitoa kwa mkopo kwenye timu aliyokuwa anaifundisha Singida United ambako nikapata namba kikosi cha kwanza, nikapambana na kuushawishi uongozi wa Azam na kuamua kunirudisha tena,” anasema.

KIRAKA ISIPOKUWA KIPA

Katika kazi yoyote kunakuwa na vitengo maalumu kila mmoja anakuwa na jukumu lake mfano mwalimu kuna anayefundisha somo la kiswahili, mwingine kiingereza wakati kwenye tasnia ya habari kuna waandishi wa siana na michezo japo kuna wengine wanaweza kufanya zote hata kwenye soka ni vivyohivyo, kuna wanaocheza kiungo, beki, mshambuliaji kwa anayeweza namba zote anaitwa kiraka.

Basi unaambiwa mbali na nafasi ya kiungo aliyozoeleka kucheza Mudathir ni fundi wa kucheza nafasi ya ushambuliaji yaani namba 10, pia anaweza akacheza winga na namba nane na namba sita ambayo ndio anayoifurahi zaidi akiitimumikia.

“Nilipokuwa mdogo nilikuwa nacheza nafasi ya ushambuliaji baadaye nikabadilishwa na kucheza winga, namba 10, nane na sasa nacheza sita namba ambayo naifurahia kwani nacheza kwa kujiamini na kujiachia zaidi,” anasema.

STARS YAMPA REKODI MBAYA

Wakati nyota wengi wa soka hasa wanaochipukia kucheza ndoto zao kubwa ni kuona siku moja wanaitwa kwenye vikosi vyao vya timu ya taifa, lengo likiwa ni kupambania nchi zao basi unaambia Mudathir Taifa Stars imemvunjia rekodi.

“Tangu nimeanza kucheza soka ni mara moja tu ndio nilionyeshwa kadi nyekundu na sio kwenye klabu ninayoichezea ni kwenye Timu ya Taifa ‘Taifa Stars’,” anasema.

“Nimecheza soka la ushindani Azam FC na Singida United sijawahi kuonyeshwa kadi nyekundu mara ya kwanza kuonyeshwa ni kwenye mchezo wa Stars dhidi ya Algeria,” anasema Mudathir.

Maisha ya soka kwa mchezaji ni popote, kikubwa wanachokiangalia ni fedha ambazo ndio zinawafanya waweze kuendesha maisha yao ya kila siku mchezaji anaweza akatoka Ligi Kuu na baadaye akaenda Ligi Daraja la Kwanza yote ni kufuata maslahi.

Mudathir ambaye amethibitisha kuwa alianza kucheza soka mwaka 2013 ametoa tofauti ya timu mbili alizochezea Azam na Singida United kulingana na namna alivyoishi kwenye timu hizo.

“Azam ni timu nzuri na kubwa ina kila kitu, Singida United ilikuja na ikavuma mwaka mmoja na sasa imepotea kama sio kuyumba kiushindani ila Azam bado ipo na inaendelea kupambana kuonyesha ushindani huwezi kuifananisha na Singida,” anasema.

MSHAHARA UMEMPA NYUMBA

Soka ni biashara, hivyo ndivyo unavyoweza kusema kutokana na namna linavyowanufaisha wachezaji ambao kwa sasa wengi wao wanamiliki mali zao wenyewe kama nyumba, magari na biashara mbalimbali.

“Soka linalipa kwa wapambanaji na waliolifanya kama kazi kama zilivyo kazi nyingine, kwa upande wangu limenilipa japo sio sana kwani nakumbuka mshahara wangu wa kwanza ulinisaidia hadi sasa namiliki nyumba,” anasema.

“Nakumbuka mshahara wangu wa kwanza ulikuwa ni laki mbili na nusu nilikuwa na mahitaji mengine ya kujenga nyumba, hivyo hiyo niliyoipata iliongezea mahitaji ambayo yalikamilisha ujenzi,” anasema Mudathir.

BADO ANALIDAI SOKA

Kila mwanadamu ana malengo aliyojipangia kwa kile anachokifanya wakati huo kwa wanafunzi wengi wao wanatamani kuhitimu elimu na kuingia hatua inayofuata kama ni msingi, basi atatamani kwenda sekondari na sekondari anatamani kwenda chuo, basi hata kwenye soka ni hivyohivyo.

Wachezaji pia wamejiwekea malengo kuna wanaotamani kucheza Ligi Daraja la Kwanza na wengine Ligi Kuu huku wengine wakitamani kutoka taifa moja kwenda jingine, ndivyo anavyobainisha kiungo wa Azam FC ambaye amethibitisha kuwa bado analidai soka.

“Nimecheza soka la ushindani miaka tisa sasa siwezi kusema limenilipa kwani bado sijatimiza malengo yangu, bado nalidai na naamini linaweza kunilipa kutokana na juhudi zangu binafsi,” anasema.

MUDATHIR AMUIBUA

GODFREY BONY

Katika kila jukumu kila mwanadamu ana mtu ambaye alimvutia na kutamani kuwa kama yeye kuna wanaosomea ualimu na wanakuwa na waalimu ambao wanatamani kufikia mafanikio yao ndivyo ilivyotekea kwa Mudathir.

Anasema akiwa na umri mdogo alikuwa anavutiwa na kiungo wa zamani wa timu ya Yanga, Tanzania Prisons na Taifa Stars, marehemu Godfrey Bony ambaye alicheza kwa mafanikio kwenye timu hizo.

“Nilikuwa navutiwa na uchezaji wa Bony, Mwenyezi Mungu amlaze mahala pema peponi na ampunguzie adhabu ya kaburi, nitaendelea kufuatilia video zake na kujifunza pale ninapoamini sipo sahihi,” anasema na kuongeza kwa wachezaji wa Azam anamkubali zaidi Aggrey Morris.

KAMA SI SOKA ANGEUZA UROJO

Kila mwanadamu huwa anajipangia majukumu na akiwa bado ana umri mdogo kwa kuamini kuwa akikua atayatekeleza lakini sio wote wanafanikiwa kutimiza ndoto zao hizo kulingana na ukuaji wao.

Mudathir ameweka wazi kuwa tangu mdogo alikuwa anapenda kucheza mpira lakini hakuwa na imani kama ndio ungemtoa kimaisha zaidi aliamini katika biashara lakini imekuwa tofauti.

“Malengo yangu ilikuwa ni kuwa mfanyabiashara mkubwa Zanzibar lakini Mungu alinionyesha kuwa njia sahihi ya mimi kufanikiwa ni miguu yangu mwenyewe kucheza mpira na ndio maana nipo Azam FC,” anasema.

NYOTA WAKE 11 CHAMA, KAHATA NDANI

Ligi Kuu Tanzania Bara inaendelea huku kila timu ikisaka nafasi ya kuiwakilisha nchi kimataifa

kiungo wa Azam Mudathir ameonyesha hisia zake kwa nyota 11 wa soka na kuthibitisha kuwa ndio kikosi cha mataji. Anasema amecheza Ligi Kuu muda mrefu, hivyo anatambua na kuthamini uwezo wa kila mchezaji na kuamua kutengeneza kikosi chake bora ambacho amethibitisha kikiwa pamoja kinaweza kutwaa mataji kila msimu.

“Aishi Manula, Shomari Kapombe, Mohamed Hussein ‘Tshabalala’, Aggrey Morris, Kelvin Yondani, Mudathir Yahya, Abubakari Salum ‘Sure Boy’, Francis Kahata, Clautus Chama, John Bocco na Joseph Mahundi,” anasema na kuthibitisha kuwa Kocha Hans van der Pluijm.

IBADA KWANZA

Katika soka kuna changamoto nyingi, huku suala la wachezaji kupigana misumari (kurogana) likiwa tatizo ambalo linawatoa mchezoni wengi na wengine wakifikia uamuzi wa kuachana na mchezo huo kutokana na ushirikina. Inaaminika ushirikina upo michezoni japokuwa si wote wanaoamini suala hilo.

“Sijawahi kulogwa na siamini katika kulogana naamini kwenye upambanaji kujituma kufanya mazoezi kwa wakati huku nikimuomba Mungu afanikishe kile ninachotamani kukifanya kwa wakati,” anasema.

“Mimi ni mtoto wa Kiislam naamini katika swala naswali sana na nimekuzwa katika mazingira ya dini, hivyo kila jambo nalifanya nikiamini Mungu yupo na ndiye msaada wangu na sio kitu kingine chochote,” anasema Mudathiri ambaye ni mwenyeji wa Zanzibar.