Mtunisia Simba akabidhiwa mastaa 13

KIKOSI cha bingwa mtetezi wa Ligi Kuu Bara, Simba jioni ya leo Oktoba 4, 2020 kitakuwa Uwanja wa Jamhuri Dodoma kutafuta pointi tatu dhidi ya wenyeji wao JKT Tanzania, huku kocha wa viungo wa timu hiyo akikabidhiwa mastaa 13 ili kuwaweka fiti kabla ya kuvaana na watani wao, Yanga Oktoba 18.

Simba inaongoza kwa kutoa nyota 14 walioitwa timu mbalimbali za taifa, wengi wakiwa ni wa kikosi cha kwanza akiwamo kipa Aishi Manula, Shomary Kapombe, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’, Jonas Mkude, Said Ndemla, Mzamiru Yasin na John Bocco, walioitwa Taifa Stars sambamba na wale wa kigeni waliotwa na nchi zao.

Luis Miquissone wa Msumbiji, Larry Bwalya na Clatous Chama wa Zambia na Wakenya, Francis Kahata na Joash Onyango ni kati ya mastaa wa Msimbazi walioitwa kwenye timu zao za taifa na Kocha Mkuu wa Simba, Sven Vandenbroeck katika kuhakikisha wachezaji wote walioitwa katika timu za taifa na wale waliobaki nchini wanakuwa katika hali moja ya ushindani amewaandalia programu maalumu.

Iko hivi. Kocha wa viungo Mtunisia Adel Zrane ndiye aliyekabidhiwa mastaa 13 wa kigeni na wazawa ambao hawakuitwa timu za taifa, ili kupigishwa tizi wakati wakiwasubiri wenzao kabla ya kuvaana na Yanga katika Kariakoo Derby kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Oktoba 18.

Mechi hiyo inasubiriwa kwa hamu kutokana na matokeo ya mwisho kwenye ligi na Yanga ilishinda 1-0 kwa bao la Bernard Morrison aliyehamia Msimbazi, lakini pia Yanga ikigongwa 4-1 katika mechi ya nusu fainali ya Kombe la FA.

Akizungumza na Mwanaspoti, Zrane alisema wataendelea na ratiba ya mazoezi mbalimbali ya nguvu akiwemo (Gym) mara baada ya mechi yao dhidi ya JKT ikiwamo ya kucheza mpira kwa wachezaji 13, watakaobaki nchini.

“Tunaendelea na programu ya mazoezi kwa wachezaji hawa ambao tumebaki nao kwa sababu tatu ili kuwa sawa kiutimamu wa kimwili kwani tukitoa mapumziko kwa waliobaki wale waliokuwa katika timu za taifa watakuwa bora kwani wanafanya mazoezi na watacheza mechi,” alisema Zrane na kuongeza;

“Baada ya ratiba ya timu za taifa kumalizika inaonyesha mchezo wetu wa mbele tunacheza dhidi ya Yanga, kwa maana hiyo tunatakiwa kuwa katika hali ya maandalizi ya kutosha kwa wachezaji wote. Naimani programu hii inaweza kutusaidia kama ambavyo ilikuwa msimu uliopita kipindi timu za taifa zinaendelea na majukumu yao nasi tulikuwa tunafanya mazoezi na wachezaji wachache ili wakija kuungana kusiwe na tofauti kubwa.”

Wachezaji hao 13 watakaoliamsha dude na Zrane wakati wenzao wakiwakilisha nchi kwenye mechi za kirafiki za kimataifa zinazotambuliwa na FIFA kwa timu zao za taifa ni Benno Kakolanya, Ally Salim, David Kameta na Gadiel Michael.

Wengine Pascal Wawa, Ibrahim Ame, Erasto Nyoni, Kennedy Juma, Chriss Mugalu, Bernard Morrison, Hassan Dilunga, Ibrahim Ajibu na Charles Ilanfia.