Mtoko wa Klopp dirisha hili la usajili

Muktasari:

Daniel Sturridge anaondoka na kutokana na hilo Klopp ana majina ya washambuliaji 12 ambao anawafuatilia mmoja baada ya mwingine na kwenye dirisha hili la usajili kuna mmoja hapo atatua Anfield kufanya mambo.

LIVERPOOL,ENGLAND.LIVERPOOL wataingia sokoni kusaka fowadi wapya kwenye dirisha hili la majira ya kiangazi huko Ulaya.

Hata hivyo, Kocha Jurgen Klopp mpango wake ni hataki kutumia pesa nyingi sana katika kuboresha safu yake ya ushambuliaji baada ya kuwa na wakali wengine kama Divock Origi na Rhian Brewster, ambao wanaoongezea nguvu kwenye ile fowadi ya Sadio Mane, Roberto Firmino na Mohamed Salah.

Daniel Sturridge anaondoka na kutokana na hilo Klopp ana majina ya washambuliaji 12 ambao anawafuatilia mmoja baada ya mwingine na kwenye dirisha hili la usajili kuna mmoja hapo atatua Anfield kufanya mambo.

Bertrand Traore - Lyon

Staa wa zamani wa Chelsea ambaye alienda kwa mkopo Ajax na Vitesse kabla ya kunaswa jumla na Lyon. Winga Traore ni balaa anapokuwa uwanjani huku kasi yake ndicho kitu kinachowavutia Liverpool na kuhitaji saini yake. Umri wake ndio kwanza miaka 23.

Maxwel Cornet - Lyon

Staa mwingine wa Lyon kwenye orodha hii ya wakali wanaosakwa na Liverpool kwa nguvu zote. Cornet amekuwa na kiwango bora kabisa hasa kwenye kufunga mabao na hilo ndilo linalomfanya Kocha Klopp kuhitaji saini yake akaongeze nguvu kwenye fowadi yake Anfield.

Samuel Chukwueze - Villarreal

Winga w Kinigeria, Chukwueze ni moja ya makinda wanaosumbua kwenye soka la Ulaya kwa sasa. Staili yake ya uchezaji imemfanya afananishwe na Arjen Robben huku panga pangua akipata namba Villarreal kiasi cha kuwafanya Liverpool kutaka huduma yake matata.

Ryan Fraser - Bournemouth

Fraser anakumbukwa vizuri na mashabiki wa Liverpool kwa kile alichowafanya Desemba 2016 na alitokea benchi kuja kupindua matokeo ya kipigo cha 3-1 kuwa ushindi wa 4-3. Liverpool sasa wanamtaka staa huyo ambaye pia anahusishwa na Arsenal na Man United.

Hakim Ziyech - Ajax

Moja ya wachezaji waliocheza soka la kiwango cha juu sana kwenye kikosi cha Ajax msimu huu. Jambo hilo limemfanya Ziyech kuzungumziwa na klabu kubwa zote za Ulaya huku Liverpool wakihitaji saini yake akafanye kazi huko Anfield na kina Sadio Mane.

Timo Werner - RB Leipzig

Straika huyo wa Kijerumani kwa muda mrefu sana amekuwa akihusishwa na Liverpool lakini uhamisho huo umeshindwa kukamilika.

Uwezo wake wa kufunga mabao ndicho kitu kinachowavutia Liverpool wakitaka kumwonyesha kwenye safu yao ya ushambuliaji.

Joao Felix - Benfica

Ni staa wa aina yake na hakika ni mchezaji atakayewagharimu pesa nyingi zaidi Liverpool katika kupata saini yake. Kinda huyo amekuwa akiwindwa na timu nyingi huku imedaiwa saini yake kuipata ni Pauni 105 milioni. Klopp itabidi ajipange kwelikweli kumnasa Felix.

Nicolas Pepe - Lille

Manchester United na Arsenal zimetajwa kuvutiwa na winga wa Ivory Coast, Nicolas Pepe, ambaye amekuwa na kiwango bora kabisa huko kwenye Ligue 1 msimu. Lakini, Liverpool ndio wanaonekana kumhitaji zaidi staa huyo aje kuwaongezea makali zaidi.

Julian Brandt - Bayer Leverkusen

Kocha Jurgen Klopp hana kificho juu ya mapenzi yake kwa staa huyo wa Kijerumani na mpango wake ni kuhakikisha anamvuta mchezaji huyo Anfield.

Brandt anajipangaa kwenda Borussia Dortmund kuziba pengo la Christian Pulisic, lakini Klopp anaweza kupindua meza.

David Neres - Ajax

Staa mwingine wa Ajax kwenye orodha hii. Nyota wa Kibrazili, Neres amekuwa kwenye kiwango bora kiasi cha kumfanya afukuziwe na klabu nyingi vigogo ikiwamo Real Madrid, Chelsea na Arsenal. Liverpool wanaonekana kuwa siriazi wakimtaka staa huyo atue kwao.

Felipe Anderson - West Ham

Staa wa Kibrazili aliyeonyesha mambo makubwa kwenye Ligi Kuu England msimu huu. Kiwango chake matata huko West Ham United kimemfanya Felipe Anderson kuingia kwenye rada za Liverpool. Shida inakuja sehemu moja tu, West Ham hawataruhusu aondoke.

Maxi Gomez - Celta Vigo

Mapema mwaka jana, Liverpool waliulizia mpango wa kumchukua staa wa Celta Vigo, Maxi Gomez. Hata hivyo, baadaye walipunguza kasi yao kwenye kumfukuzia mshambuliaji huyo huku Arsenal nao wakiingia kwenye orodha yao wakitaka huduma yake.