Mtibwa yachapwa, Katwira atoa neno

Wednesday September 12 2018

 

By Juma Mtanda

Morogoro. Kocha mkuu wa Mtibwa Sugar, Zubery Katwira ametoa mchongo kwa Mawenzi Market FC kutekeleza mambo ya msingi kama inataka kufanya vizuri katika ligi daraja la kwanza msimu huu ili kupata nafasi ya kutinga Ligi Kuu Tanzania bara msimu ujao.

Akizungumza na MCL Digital baada ya kumalizika kwa mchezo wa kirafiki kati ya Mtibwa na Mawenzi Market FC kwenye Uwanja wa Jamhuri Morogoro jana, Katwira alisema ili Mawenzi Market FC iweze kufanya vyema katika michezo ya ligi daraja la kwanza msimu huu wanapaswa kuungana na kuwa kitu kimoja kuanzia benchi la ufundi, wachezaji na uongozi.

Katwira alisema Mawenzi FC imefanikiwa kuwafunga bao 1-0 dakika za mapema na kuhimili kasi, kuondoa hofu na mikimiki ya wachezaji wengi wenye vipaji wa Mtibwa Sugar hilo wanapaswa kuzingatia kutokana na maelekezo ya walimu wao na watafika mbali.

Naye kiungo mshambuliaji wa Mtibwa Sugar, Haruna Chanongo alisema anaiona Mawenzi Market FC ikiwa tofauti na msimu uliopita na endapo viongozi wa chama cha soka mkoa wa Morogoro na uongozi wa klabu bila washaka watafikisha malengo.

“Nimewaona Mawenzi Market FC ile ya msimu uliopita na msimu huu naona hii ya msimu huu inaweza kutimiza malengo endapo tu uongozi chama cha soka mkoa na uongozi wa timu pamoja na wachezaji wanaweza kufanya jambo.”alisema Chanongo.

Mashabiki waendelee kuwaunga mkono wachezaji na wasiwakatishe tamaa kwani ameona Market Market FC ikicheza kwa nguvu na uelewano na wanapaswa kuongeza kasi ili kuwachanganya maadui zao,” alisema Chanongo.

Kocha mkuu wa Mawenzi Market, Mussa Rashid alisema timu yake inahitaji kucheza michezo ya kirafiki mmoja au miwili kabla ya kuanza ligi daraja la kwanza.

Mawenzi wataanza kutupa karata yao kwa mchezo wa ufunguzi na Mufindi FC Septemba 29 mwaka huu katika Uwanja wa Jamhuri Morogoro.

Rashid alisema kwa sasa anatafuta kucheza michezo miwili ya kirafiki baada ya kucheza michezo 10 kwani itamsaidia kupata mwelekeo wa kupata kikosi bora chenye ushindani ili kupata matokeo mazuri ya kusaka nafasi ya kucheza ligi kuu msimu ujao.

Advertisement