Mtibwa kujiuliza kwa Namungo

LIGI KUU BARA raundi ya saba itaendelea leo Jumatatu Oktoba 19, 2020 ambapo mechi nne zitatimua vumbi katika viwanja tofauti.

Mechi ya kwanza ambayo itaaanza saa 8:00 mchana JKT Tanzania watakuwa nyumbani katika Uwanja wa Jamhuri, Dodoma dhidi ya Tanzania Prisons, baada ya hapo kutakuwa na mechi nyingine tatu ambazo zote zitaanza saa 10:00 jioni.

Mechi hizo ni Mtibwa Sugar watakuwa Uwanja wa Jamhuri, Morogoro kucheza dhidi ya Namungo ikiwa ni siku moja tangu kuondokewa kwa kocha mkuu Zuberi Katwila aliyejiunga na IhefuSC wakati Coastal Union watakuwa nyumbani CCM Mkwakwani, Tanga dhidi ya Biashara United na Polisi Tanzania ambao watakuwa nyumbani dhidi ya Gwambina.

Ukiachana na mechi hizo za leo kesho Jumanne Oktoba 20 kutakuwa na michezo mingine mine.

Mechi ya kwanza itaanza saa 8:00 mchana Ruvu Shooting watawakaribisha KMC, Mwadui FC nao watakuwa nyumbani dhidi ya Mbeya City ambao wanaburuza mkia katika msimamo na Kagera Sugar ambao watakuwa Uwanja wa Kaitaba, Kagera watacheza na Namungo.

Ukiachana na mchezo huo mechi ya nne ambayo itafatiliwa zaidi na mashabiki wengi wa soka hapa nchini ni ile ya Ihefu ambao watakuwa nyumbani kucheza dhidi ya vinara wa ligi Azam FC.

Kocha mpya wa Ihefu, Zubery Katwila anakibarua kigumu katika mechi yake ya kwanza atakapokutana na Azam FC, katika pambano ambalo litachezwa Uwanja wa Sokoine, Mbeya kuanzia saa 10:00 jioni.

Katwila ataiongoza Ihefu ambayo katika mechi sita za Ligi Kuu Bara walizocheza wameshinda moja, hawajatoka sare, wamefungwa tano, wamefungwa mabao nane, wamefunga mawili na pointi ambazo wamekusanya ni tatu.

Kwa upande wa wapinzani wao Azam FC, wameanza kwa kasi ya kupata matokeo mazuri msimu huu wanaongoza ligi wakiwa na pointi 18, wameshinda mechi zao zote sita, hawajapoteza wala suluhu, wamefunga mabao 12 na wao kufungwa mawili.

Mtihani mwingine ambao Katwila atakwenda kukutana nao safu yake ya ulinzi imeruhusu kufungwa mabao 12, wakati mastraika wawili wa Azam, Prince Dube kinara wa ufungaji katika ligi akiwa na mabao sita na Obrey Chirwa amefunga manne na wawili hao wamefunga jumla ya mabao kumi mpaka sasa.

Katwila alisema ameamua kuondoka Mtibwa Sugar aliyoitumikia kwa miaka 20, kucheza na kuifundisha kutokana na kubadili upepo mbaya ambao ulikuwa unamkabili jambo ambalo lilipelekea hata baadhi ya watu kumwambia amemaliza hana jipya tena la kutoa kwa wachezaji wake.

"Nimekuja hapa Ihefu kutafuta changamoto mpya kwani nafahamu timu hii haijafanya vizuri mpaka wakati huu lakini naimnai ushirikiano ambao nimeonyeshwa kutoka kwa viongozi pamoja na wachezaji naweza kuinua na kufikia katika mafanikio," alisema.

"Naanza kazi ya kuiongoza Ihefu katika mechi ngumu dhidi ya Azam ambao wapo vizuri msimu huu muda ambao nimeandaa timu ili kuwakabiri wapinzani ni siku mbili kuna mbinu na vitu vya kiufundi ambavyo nimewapatia ili kwenda kuwakabiri.

"Kama wachezaji wangu wataweza kuyafanyia kazi vizuri maelekezo hayo tunaweza kupata matokeo mazuri dhidi ya Azam ingawa tunafahamu si jambo rahisi tunatakiwa kulifanyia kazi kwa nguvu zote ndani ya dakika 90, lakini mara nyingi timu ambayo hubadilisha kocha mechi ya kwanza huwa inaanza vizuri," alisema Katwila ambaye amechukua mikoba ya kuinoa Ihefu kutoka kwa Maka Mwalwisi.

Ofisa habari wa Azam, Thabit Zakaria alisema amezungumza na kocha wao Aristica Cioaba na amemueleza kimbinu Ihefu wapo chini yao ila wanaweza kuingia kwa kubadilika kutokana wakataka kushindana kutokana na kubadilisha kocha, matokeo mabaya na wanacheza nyumbani.

"Cioaba ameniambia Ihefu wanaweza kuwa bora na kucheza vizuri kama ambavyo ilivyokuwa mechi yao na Simba wameliona hilo lakini hata uwezo wa mchezaji mmoja mmoja unaweza kuamua matokeo ya mechi hii," alisema Zakaria.