Mtibwa Sugar kucheza tatu nje ya nchi

Muktasari:

Kikosi cha Mtibwa Sugar kimeamua kufanya maandalizi yake ya Kombe la Shirikisho Afrika kwa kucheza mechi tatu za kirafiki za kimataifa.

Dar es Salaam. Mabingwa wa Kombe la FA, Mtibwa Sugar kimepanga kufanya maandalizi ya mashindano ya Kombe la Shirikisho Afrika kwa kucheza mechi tatu za kimataifa za kirafiki na michezo ya Ligi Kuu Bara kama kipimo.

Wawakilishi hao wa Tanzania msimu huu waliondoka katika mashindano hayo zaidi ya miaka 10 na sasa wamerudi kwa kasi mpya.

Mkurugenzi wa Ufundi wa Klabu ya Mtibwa Sugar, Salum Mayanga amesema mpango huo utakwenda kuleta mafanikio makubwa katika timu yao.

"Tumejipanga katika mambo mawili kabla ya kuingia katika mashindano ya kimataifa. Si muda mrefu tutataja nchi ambazo zitatoka timu hizo na zipo tutakazocheza nyumbani na ugenini,"alisema Mayanga ambaye aliichezea timu hiyo na kuwa kocha mkuu miaka ya nyuma.

"Kwa sababu ligi yetu ina timu nzuri zenye hadhi ya kimataifa hivyo katika mechi tutakazocheza nao, zitakuwa sehemu yetu ya maandalizi."

Mbali na kucheza na kuifundisha Mtibwa Sugar, Mayanga alizifundisha Kagera Sugar na Tanzania Prisons kabla ya kupewa majukumu ya kuifundisha Taifa Stars.