Mtasubiri sana kwa Prisons

Muktasari:

  • Kocha huyo aliyenyakuliwa na Prisons kuziba nafasi ya Mohammed Abdallah ‘Bares’ aliliambia Mwanaspoti hawana kikosi kibovu, bali upepo mbaya uliowapitia lakini hivi sasa hali ndani ya timu yake imetulia ndiyo maana wameanza kupata matokeo mazuri.

KAMA kuna shabiki anawaza kuiona Prisons ikishuka daraja msimu huu, pole yake kwani kocha mkuu wa timu hiyo, Mohammed ‘Adolf’ Rishard amesema hashuki mtu.

Kocha huyo aliyenyakuliwa na Prisons kuziba nafasi ya Mohammed Abdallah ‘Bares’ aliliambia Mwanaspoti hawana kikosi kibovu, bali upepo mbaya uliowapitia lakini hivi sasa hali ndani ya timu yake imetulia ndiyo maana wameanza kupata matokeo mazuri.

“Nimeikuta Prisons katika hali mbaya sijajua nini kilikuwa kinawapa shida, kikubwa ninachoweza kukisema wana kikosi kizuri hakuna mabadiliko au miujiza niliyoifanya zaidi ya kubadili mfumo ambao kwa namna moja au nyingine umenibeba.”

“Tunasogea kutoka kushinda mchezo mmoja hadi sasa tumefikia michezo minne, lolote linawezekana lakini kikubwa ninachokiangalia ni kubaki Ligi Kuu na inawezekana kwa michezo iliyobaki kama tutapata matokeo mazuri,” alisema

Rishard aliongeza mzunguko wa pili wa ligi waliopo sasa timu nyingi zilizo kwenye nafasi mbaya zinapambana kujinasua hivyo bado ana wakati mgumu kuinasua timu hiyo iweze kubaki