Mtanzania aomboleza kifo cha bosi wa Leicester City

Muktasari:

  • Ben alisema ubingwa ule, ulikuwa kama wa timu za vijana maana walipata nafasi ya kuusheherekea na kikosi cha kwanza kwenye Uwanja wa King Power.

KINDA la Kitanzania, Ben Anthony Starkie anayeichezea timu ya vijana ya Leicester City chini ya umri wa miaka 16 nchini England, ameungana na wenzake kuomboleza kifo cha bilionea na mmiliki wa klabu hiyo, Vichai Srivaddhanaprabha.

Klabu ya Leicester City, ilithibitisha kuwa, Vichai (60), kutoka Thailand, wafanyakazi wake wawili, rubani na abiria mmoja walifariki baada ya ndege aina ya elikopta waliyopanda kuanguka.

Ben alisema hakika, Vichai hawezi kusahaulika na atabaki kwenye kumbukumbu za wapenzi wa soka na mashabiki wa Leicester City ambao kiu yao ilikatwa kwa kuchukua Ubingwa wa Ligi Kuu England msimu wa 2015/16.

“Mpira wa Ulaya unategemea fedha kwa hiyo kama asingeamua kuichagua Leicester na kuwekeza ina maana tusingekuwa mabingwa wa ligi, kila mmoja wetu wameumizwa na kifo chake, simanzi imetanda kwenye mji wetu,” alisema Ben.

Alisema kifo cha bilionea huyo kimemfanya kukumbuka namna alivyopata nafasi kwa mara ya kwanza kulishika taji la Ligi Kuu England.

Ben alisema ubingwa ule, ulikuwa kama wa timu za vijana maana walipata nafasi ya kuusheherekea na kikosi cha kwanza kwenye Uwanja wa King Power.

HUYU NDIYE VICHAI

Bilionea Srivaddhanaprabha, 60, alikuwa ameoa na kujaliwa watoto wanne.

Alinunua Leicester City kwa £39m mwaka 2010 na akawasaidia kulipa madeni kisha kupanda ngazi hadi kucheza Ligi Kuu miaka minne baadaye.

Chini ya umiliki wake, klabu hiyo ilishinda taji la Ligi Kuu 2016 baada ya kuanza msimu ikiwa haipigiwi upatu.

Vichai alikuwa mwenyekiti wa kampuni ya maduka yasiyotoza kodi ya King Power International Group ambapo ndipo jina la uwanja wa Leicester linatoka, na pia jina la mdhamini kwenye jezi zao.

Utajiri wake unakadiriwa $3.8bn (£2.9bn), na anakadiriwa na Forbes kuwa mtu wa nne kwa utajiri huko Thailand.