Mtanzania amtembezea mzungu kipigo cha maana Ulaya

Muktasari:

  • Mtanzania huyo aliwaduwaza Waengland ambao walikuwa ni maelfu ya mashabiki ambao walifika kwa ajili ya kumshangilia Eggington katika raundi ya pili tu baada ya kumchapa mpinzani wake ngumi 51, bila majibu hadi mwamuzi Kevin Parker alipomwokoa katika pambano hilo lililokuwa la raundi 10 la uzani wa super welter.

Dar es Salaam. Bondia Mtanzania, Hassan Mwakinyo amefanya mambo makubwa ukumbi wa  Barclaycard Arena kule Birmingham, England baada ya kumchapa, Sam Eggington ambaye ni raia wa nchi hiyo hadi akaokolewa na mwamuzi.
Mtanzania huyo aliwaduwaza Waengland ambao walikuwa ni maelfu ya mashabiki ambao walifika kwa ajili ya kumshangilia Eggington katika raundi ya pili tu baada ya kumchapa mpinzani wake ngumi 51, bila majibu hadi mwamuzi Kevin Parker alipomwokoa katika pambano hilo lililokuwa la raundi 10 la uzani wa super welter.
Video ya pambano hilo ilionyesha ushindi wa Mtanzania ulikuwa mapema katika raundi ya kwanza kutokana na makonde aliyompa mpinzani wake.
Eggington alilazimika kutumia dakika moja ya mapumziko kugangwa ili kupunguza maumivu huku kitendo hicho kikiamsha morali ya Mwakinyo ambaye alizunguka kwenye kona zote za ulingo akitamba.
Mwamuzi Parker alitakangaza matokeo ya Technical Knock Out (TKO) kwa Mwakinyo ambaye kabla ya ushindi huo, alikuwa na pointi 25 huku mpinzani wake akiwa na pointi 145 za ubora wa ngumi duniani.
Baada ya ushindi huo, Mwakinyo amepata 'shavu' kwa kwenda kuzichapa pambano la kuwania ubingwa wa kimataifa wa IBF kwa vijana katika uzani wa super middle dhidi ya Wanik Awdijan.
Pambano hilo limepangwa kufanyika Oktoba 20 kwenye ukumbi wa Alex Sportcentrum, Nuremberg katika mji wa  Bayern, nchini Ujerumani.