Mtanzania aingia anga za Caster Semenya AAG

Muktasari:

Mtanzania huyo amekuwa na rekodi ya kufanya vizuri na kushinda medali kadhaa katika mashindano ya Afrika Mashariki na Kati ya vijana chini ya miaka 18.

Dar es Salaam. Mwanariadha wa Tanzania, Regina Mpigachai ni miongoni mwa nyota watakaochuana kusaka medali ya dhahabu ya mbio za mita 800 katika Michezo ya Afrika (AAG) ambayo bingwa mtetezi ni mwanaridha wa Afrika Kusini, Caster Semenya.

Michezo hiyo itafunguliwa Agosti 19 kwenye uwanja wa Stade Olympique - Complexe Sportif Prince Moulay Abdellah uliopo Rabat huku mfalme wa Morocco, Mohammed VI akitarajiwa kuwa mgeni rasmi.

Katika michezo hiyo, Tanzania itawakilishwa na wanariadha sita akiwamo Regina ambaye atachuana katika mbio za mita 800, ambazo kwenye michezo iliyopita ya 2015 iliyofanyika kwenye Uwanja wa New Kintele, Congo Brazzaville, Semenya aliibuka kidedea.

Hata hivyo, Regina ambaye ni kinda wa timu ya vijana amejumuishwa kwenye kikosi cha wakubwa kushiriki michezo hiyo ambayo itakuwa ni mara yake ya kwanza ana rekodi ya kukimbia na kumaliza mbio hizo kwa dakika 2:10:51.

Semenya hivi karibuni rufaa yake CAS ilitupiliwa mbali akitakiwa kumeza dawa kupunguza kiwango cha homoni ambacho kilielezwa alichonacho ni cha juu na hata wanawake wenzake wakimbie vipi hawawezi kumfikia alishinda medali ya Afrika msimu uliopita akitumia dakika 2:00.97.

Muda huo ni sekunde 9 zaidi mbele ya Regina, huku Annet Mwanzi wa Kenya aliyekimbia kwa dakika 2:01.54 na Chaltu Shume wa Ethiopia aliyekimbia wakitwaa medali ya fedha na shaba kwenye michezo ya msimu uliopita.

"Sina hofu ya ushindani, najua ni mashindano magumu na yanashirikisha wanariadha wakongwe, namfahamu Semenya ni mwanariadha maarufu duniani, lakini hicho hakiwezi kuwa kikwazo kwangu kama ikitokea nikashindana naye," alisema Regina.