Mtanzania agomewa kuzichapa Uingereza

Thursday June 27 2019

 

By Imani Makongoro

BONDIA Mtanzania, Flora Machela amegomewa kucheza nchini Uingereza na Bodi ya Ngumi za Kulipwa ya nchi hiyo.

Machela ambaye alikuwa amefuatana na wakala wake, Nassoro Rashid ‘Chid’ alishindwa kucheza nchini humo kutokana na rekodi yake ya kupigwa mfululizo.

“Promota hakuwa na tatizo, isipokuwa mamlaka ya ngumi nchini humo ilimkataa asicheze siku chache kabla ya pambano tukiwa tayari Uingereza,” alisema wakala wa pambano hilo, Chid.

Alisema chama hicho kilidai rekodi za bondia huyo Mtanzania siyo nzuri kwani amepigwa kwa KO nchini Australia, kisha Ujerumani, Nairobi na Zambia.

Rekodi zinaonyesha Machela amepigwa kwa KO mara nne mfululizo ambapo alipigwa na Catherine Phiri kwa KO, Fatuma Zarika KO, Lauryn Eagle TKO na Derya Saki TKO.

“Machela yeye alikuwa tayari kucheza, lakini Bodi ya Ngumi Uingereza ndiyo ilimkataa na siyo promota, hivyo mpinzani wake akabadilishiwa bondia na sisi tukalazimika kurudi nchini,” alisema Chid.

Advertisement

Alisema hata hivyo, promota wa Uingereza amewataka wajipange upya na kuahidi kuwapa pambano jingine Julai 20 kwani Machela alikuwa tayari kwa pambano na alifanya vipimo vyote na kufuzu, isipokuwa Bodi ya Ngumi ilimgomea kutokana na rekodi ya kupigwa KO mara nyingi mfululizo.

Kocha wa Machela, Mbarouk Heri alisema hajui nini kilitokea hadi bondia wake kushindwa kucheza wakati alikuwa ameshafika Uingereza.

“Nashangaa hata sielewi tatizo ni kitu gani, isipokuwa wakala alinieleza tu kwamba eti rekodi yake siyo nzuri, sasa sijui ilikuwaje hadi wakampeleka Uingereza, ila mwenye majibu sahihi ni wakala aliyefuatana naye,” alisema kocha huyo na bondia wa zamani.

Advertisement