Mtanzania Portsmouth azipa neno Serikali, TFF

Monday February 18 2019

 

By Eliya Solomon

Dar es Salaam.Tanzania ina hazina ya kutosha ya wachezaji wenye vipaji wanaocheza soka ya kulipwa nje ya nchi na mmoja wao ni Haji Mnoga.
Mnoga ni miongoni mwa wachezaji wanaofanya vyema nje ya nchi na haikushangaza kinda huyo aliposajiliwa na Portsmouth ya England.
Portsmouth inayoshiriki Ligi Daraja la Pili, imewahi kucheza Ligi Kuu England.
Mnoga anayecheza nafasi ya beki wa kulia na kati, ameingizwa katika kikosi cha kwanza baada ya kuaminiwa na kocha Kenny Jackett.
Portsmouth ina utamaduni wa kuwatumia wachezaji wanaotoka Afrika. Awali, walikuwepo akina Nwankwo Kanu (Nigeria), Sulley Muntari na Kevin-Prince Boateng wanaotoka Ghana.
Portsmouth yenye maskani Fratton Park ni mabingwa mara mbili wa Kombe la FA walilotwaa mwaka 1939 na 2008.
Mnoga, kinda mwenye miaka 17, sasa anafuata nyayo za Kanu, aliyekuwa mshambuliaji nyota wa Nigeria enzi zake kabla ya kutundika daluga.
“Ingawa nina umri mdogo nashukuru Mungu inatia moyo kuona kocha anaanza kuniamini na kunipa nafasi ya kucheza, sina nafasi kubwa ya kucheza mara kwa mara kwenye kikosi chake, lakini utafika muda wangu nitacheza.
“Huu ni mwanzo mzuri kwangu ambacho nimekuwa nikikifanya ni kutumia vizuri nafasi ambazo nimekuwa nikipata, furaha yangu haikuelezeka nilipocheza mchezo wa kwanza,” anasema Mnoga.
Mnoga ni chipukizi wa Tanzania ambaye amekuwa na maendeleo mazuri kwenye klabu hiyo kiasi cha kuanza kupata nafasi ya kucheza katika kikosi cha Portsmouth.
Mnoga ambaye baba yake ni Mtanzania akitokea Zanzibar na mama Muingereza, anasema mkakati wake ni kuipa mafanikio Potsmouth katika mashindano inayoshiriki.
Baba wa mchezaji huyo, aliwahi kucheza timu ya Taifa ya vijana Zanzibar chini ya miaka 17 kabla ya kuachana na soka na kujikita kwenye shughuli nyingine.
Baada ya kuzaliwa Mnoga, Aprili 16, 2002 alipata elimu ya msingi Shule ya Trafalgar katika mji wa Portsmouth.
Maisha yaliendelea kwa nyota huyo kama ilivyo kwa wanasoka wengine ambao wapo kwenye mataifa yaliyoendelea akapata nafasi ya kujiunga na kituo cha soka cha Portsmouth mwaka 2008.
Mnoga alilelewa katika ngazi tofauti za soka la vijana na hatimaye Oktoba 9, 2018 akapata nafasi kwa mara ya kwanza akiwa na miaka 16 ya kucheza kikosi cha kwanza cha Portsmouth katika mchezo wa Kombe la EFL dhidi ya Crawley Town FC.
Beki huyo alicheza dakika 65 zilizotosha kuisaidia Portsmouth kuibuka na ushindi mwembamba katika mchezo walioshinda bao 1-0 kabla ya kuingia na nafasi yake kujazwa Tom Naylor.
Huo ulikuwa mwanzo wa Mnoga kuanza kuaminika na taratibu alianza  kupata nafasi ya kucheza  na hivi karibuni  alipewa tena nafasi ya kucheza kwenye robo fainali ya Kombe la EFL.
Portsmouth imetinga nusu fainali baada ya kuifunga Peterborough United bao 1-0, Januari 22  huku Mnoga akicheza dakika 56.
Katika hatua ya nusu fainali Portsmouth itakutana na Bury, Februari 26 huku mchezo wa nusu fainali ya pili ukiwa kati ya Bristol Rovers na Sunderland.
Akizungumzia uwezekano wa kucheza timu ya Taifa, ‘Taifa Stars’, Mnoga anasema inawezekana kutokana na kuwa  na asili ya Tanzania na ukizingatia hajapokea ofa yeyote kutoka England ambako amekulia.
“Naweza kucheza Tanzania tatizo kuna hili suala la uraia pacha, kama kusingekuwa na sheria zinazonibana basi ingekuwa rahisi kwangu kuamua Serikali na TFF zinaweza kuangalia suala hili kwa upana wake,” anasema beki huyo.
Kauli ya Mnoga ni ujumbe kwa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) ambalo limekuwa likihaha kusaka wachezaji bora wanaocheza nje ya nchi kuitumikia timu ya Taifa.
Mnoga ndiye mchezaji pekee wa Tanzania ambaye yupo kwenye timu ya daraja la juu zaidi England. Mwingine anayecheza soka la kulipwa nchini humo ni Adi Yussuf wa Solihull Moors ya Daraja la Nne.
Beki huyo anaweza kufuata nyazo za mastaa wa Afrika walipita Portsmouth na kufanya makubwa kwenye klabu nyingine  mfano hai ni Boateng ambaye alicheza AC Milan na sasa ametua FC Barcelona.

Advertisement