Mtango atamba kumstaafisha Miyeyusho ndondi

Muktasari:

Mtengo ana rekodi ya kupigana mapambano 17, ameshinda 14 (9 kwa KO), amepigwa mara tatu (moja kwa KO) tangu 2013, wakati Miyeyusho amepigana mapambano 60, ameshinda 42 (25 kwa KO), amepigwa 18 (15 kwa KO) ametoka sare 7 tangu 1998. 

Dar es Salaam.Bingwa wa dunia wa Universe Boxing Organisation (UBO), Salum Mtango ametamba kuhakikisha anamuondoa katika ramani ya ngumi, Francis Miyeyusho watakapozichapa Machi Mosi.

Mtango atakuwa nyumbani kwenye uwanja wa Mkwakwani mjini Tanga kumkabiri Miyeyusho bondia maarufu nchini kwenye uzani bantam.

Pambano hilo la raundi nane limeibua hisia za mashabiki wa ndondi, baadhi wakiamini ndilo litamrejesha Miyeyusho kwenye ramani ya ngumi baada ya kuwa kimya kwa muda mrefu.

Hata hivyo Mtango anayetokea kwenye kambi ya bondia namba moja Afrika kwenye uzani wa Super welter, Hassan Mwakinyo amekejeli akidai pambano hilo si la kumrejesha Miyeyusho katika ngumi, bali anakwenda kumstaafisha.

"Niko fiti, na ari na morali ya ushindi, nimetoka kuwa bingwa wa dunia karibuni, nahitaji kuendeleza rekodi ya ubingwa, Miyeyusho ni kaka yangu, namheshimu lakini ajiandae kwa kipigo," alijinasibu Mtango.

Hata hivyo Miyeyusho ‘Chichi Mawe’ ametamba kumzidi Mtango si tu uzoefu, mikanda ya ubingwa na rekodi hivyo hawezi kumsumbua.

"Mtango amedandia treni kwa mbele, siwezi kubishana naye, lakini nitamfundisha namna ngumi zinavyochezwa siku hiyo, si levo yangu katika ngumi," alitamba bondia huyo ambaye ni nembo ya mabondia wa wilaya ya Kinondoni, Dar es Salaam.

Alisema atazungumza kwa vitendo ulingoni, kwani pambano hilo limekuja wakati ambao yuko fiti.

Promota wa pambano hilo, Ally Mwanzoa alisema maandalizi yote yamekamilika na pambano litaanza saa 10 jioni kwa kiingilio cha Sh 5000 kwa wakubwa na 3000 watoto.