Mtandao FC kama zali huko Rorya

Thursday November 8 2018

By Mwandishi wetu

MTANDAO FC imetinga hatua ya Nne Bora ya Ligi Daraja la Nne Wilaya ya Rorya mkoani Mara baada ya juzi kutoka sare ya bao 1-1 na Wimbi Stars katika mpambano uliopigwa uwanja wa Nyamagaro mjini hapa.

Katika mtanange huo Mtandao waliokuwa wa kwanza kupata bao la kuongoza lililopachikwa nyavuni na straika Jangala Matiko dakika ya 30.

Kipindi cha pili, Wimbi FC waliingia uwanjani kivingine na kuongeza mashambulizi langoni mwa wapinzani wao na kusawazisha bao hilo dakika ya 60 kupitia kwa Okoth Kiberi.

Baada ya bao hilo Mtandao waliokuwa wanahitaji pointi moja kwenye mchezo huo ili kufuzu Nne Bora walianza kulinda lango lao na kuwapa wakati mgumu Wimbi FC kuweza kupata bao la ushindi.

Ushindi huo umeifanya timu ya Mtandao FC kufikisha pointi nne ambazo zimeiwezesha kutinga hatua ya Nne Bora ya Ligi hiyo.

Kocha wa Mtandao FC, Manyama Machanchu alisema baada ya kutinga hatua hiyo mipango yake sasa ni kuona timu inachuwa ubingwa wa Wilaya ya Rorya.

“Tumetinga hii hatua sasa lengo letu ni kuhakikisha tunapambana na kutwaa ubingwa wa Wilaya na hatimaye kupanda Daraja la Tatu ngazi ya mkoa,”alisema Machanchu.

Advertisement