Mtanange wa Simba, Yanga pasua kichwa

Muktasari:

Yanga na Simba zilipangwa kukutana Oktoba 18 katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara, na sasa utafanyika Novemba 07.

Dar es Salaam. Mchezo wa Yanga dhidi ya Simba uliokuwa ufanyika Oktoba 18 jijini Dar es Salaam umeahirishwa na kuzua sintofahamu.

Licha ya Bodi ya Ligi (TPLB) kudai kuwa mabadiliko hayo yametokana na ratiba ya Shirikisho la Mpira wa Miguu la Kimataifa (FIFA), bado haiingii akilini kwa wadau wa soka nchini.

TPLB ilitoa sababu za ‘kawaida’ jana kuwa ni kuwepo changamoto ya usafiri kwa baadhi ya wachezaji waliokwenda kuzitumikia timu zao za taifa, wachezaji watatu wa Simba wako kwenye timu zao za taifa.

Luis Miquissone (Msumbiji), Joash Onyango (Kenya) na Meddie Kagere (Rwanda), wameitwa katika nchi zao, huku Francis Kahata, Clatous Chama na Larry Bwalya wakiondoshwa kutokana na sababu mbalimbali.

Awali mchezo wa watani ulipangwa kupigwa Oktoba 18, siku saba baada ya mechi za kimataifa za kirafiki za kalenda ya Fifa, ambazo zinachezwa kati ya Oktoba 8,9 au 11 siku ambayo Stars itacheza na Burundi kwenye Uwanja wa Mkapa, kabla ya kusogezwa hadi Novemba 7.

Mabadiliko haya yameibua juu ya mechi ya Stars na Tunisia iliyopangwa kuchezwa Novemba 9 mjini Tunis wa kuwania kufuzu Fainali za Mataifa ya Afrika (Afcon), ingawa TFF imeeleza kuwa Stars itacheza Novemba 13, siku sita baada ya mechi ya watani.

Ingawa TFF imesisitiza kuwa ni kutokana na ugumu wa usafiri kwa wachezaji waliopo kwenye timu zao za taifa kipindi hiki ambacho dunia inapambana na janga la corona.

Kuahirishwa kwa mechi hiyo kumewashangaza vigogo wa zamani wa TFF, wakihoji kama waliofanya uamuzi huo walipitia kalenda za Fifa na CAF.

Angetile Osiah, katibu wa zamani wa TFF alisema kalenda ya Fifa na CAF ndizo zinazotoa muongozo wa mpangilio mzuri wa ratiba za ligi ya ndani ili kuepusha muingiliano wa ratiba.

“Sina uhakika kama waliofanya uamuzi huo walikuwa na kalenda za mashirikisho hayo ya kimataifa,” alisema Osiah.

Mkurugenzi wa zamani wa ufundi wa TFF, Sunday Kayuni alisema katika hilo, kuna mahala inaonyesha hakuna weledi ndani ya usimamizi.

“Kalenda ya Fifa inajulikana na sheria zake zipo wazi, inabidi kuzifuata ili kutoharibu ratiba ya ligi, japo TFF iko sahihi kwa hiki ilichokifanya,” alisema.

Mkurugenzi mstaafu wa mashindano wa TFF, Saad Kawemba alisema mechi ya timu ya taifa inapaswa kupewa thamani yake ipasavyo.

“Awali ratiba ya mechi ya Stars na Tunisia ya kuwania kufuzu kucheza Kombe la Dunia ilikuwa ichezwe Novemba 9, hivyo nilipata wasiwasi, lakini nimesikia imesogezwa mbele hadi Novemba 13, hivyo mechi ya Novemba 7 bila shaka itabaki kama ilivyopangwa,” alisema.

Kuhairishwa kwa mechi hiyo na baadhi ya mechi za ligi kuemeelezwa kuwa changamoto pia kwa klabu nyingine.

Kocha wa Mwadui FC, Khalid Adam alisema mabadiliko hayo yamekuwa yameiumiza klabu yao, ambao walijiandaa kuivaa Azam FC, Oktoba 9 na Azam imesogezwa hadi Oktoba 15.

“Tuko njia panda, hatujui kama tuendelee kubaki Dar es Salaam hadi Oktoba 15 au turudi Shinyanga, tulicheza mechi ya mwisho na Namungo mjini Ruhangwa tukaja Dar na kuambiwa mechi yetu imeahirishwa, tunaingia gharama ambazo haziko kwenye bajeti, ratiba ya ligi ni changamoto,” alisema Adam.

Ofisa Habari wa Azam FC, Thabit Zakaria ‘Zaka Zakazi’ alisema panga pangua ya ratiba imesogeza mbele mechi yao na Mwadui na ile ya Ihefu.

“Tulikuwa tupo tayari kucheza bila hata wachezaji wetu ambao wapo kwenye timu zao za taifa, lakini ndiyo hivyo,” alisema ofisa huyo.

Kocha Mecky Maxime wa Kagera Sugar alisema kusogezwa mbele kwa mechi ya watani ni kujichelewesha.

“Kwa tafsiri nyingine ina maana nje ya Simba na Yanga, timu nyingine zipo kwa ajili ya kusindikiza hii inaathiri wengine, Ulaya mambo kama haya hakuna, tujaribu kuiga huko basi,” alisema.