Mtakoma ! huku Ajibu kule Kagere

Muktasari:

  • Kati ya mabao 11 ambayo Simba imeyafunga kwenye mechi zake tisa, mabao nane imeyafungia Taifa dhidi ya timu za Prisons, Mbeya City, African Lyon na Stand United huku Kagere akinufaika zaidi kwani kati mabao matano aliyoifungia Simba hadi sasa, manne ameyapatia akicheza Dar es salaam.

STRAIKA Said Khamis anayekipiga Mbao FC amemjibu kwa vitendo Ibrahim Ajibu kwa kufunga bao kali la kideoni dhidi ya Mtibwa Sugar, lakini bado mziki wa straika huyo wa Yanga unawanyima raha mabeki na makipa wa timu pinzani.

Katika mechi saba ambazo Yanga imecheza mpaka sasa, Ajibu amehusika katika mabao 11 kati ya 14 na kumfanya awe tishio kwa mabeki wa timu pinzani kama ilivyo kwa Meddie Kagere wa Simba anavyowakosesha usingizi makipa nchini.

Achana na hizo. Kesho Jumatano na Alhamisi Ligi Kuu Bara itaendelea kwa raundi ya 10, lakini kazi itakuwa kwa mabeki na kipa wa Alliance na KMC kuhakikisha wanasalimika na umafia wa mastraika hao matata wa Simba na Yanga.

Kama Alliance waliotoka kupokea kipigo cha mabao 3-0 toka Yanga, huku Ajibu akihusika na mabao hayo yote wasipojipanga vyema watarajie kuumizwa na Kagere akisaidiana na Emmanuel Okwi na nahodha anayerejea tena baada ya kutumiki adhabua ya kifungo, John Bocco.

Alliance inayoshika mkia katika msimamo wa ligi, imekuwa na safu dhaifu ya ulinzi hasa kwa mechi za ugenini na kesho watakuwa wageni wa Simba kwenye Uwanja wa Taifa na wasipojipanga wanaenza kuzikoga nyingi.

Umakini wa kuidhibiti safu ya ushambuliaji ya Simba itakayoongozwa na Kagere ndio silaha inayoweza kuibeba Alliance vinginevyo watajikuta wakigeuzwa daraja la mafanikio kwa washambuliaji wa wapinzani wao.

Rekodi hiyo isiyoridhisha ya safu ya ulinzi ya Alliance inafanya Simba ipewe nafasi kubwa ya kuibuka na ushindi kwenye mchezo huo hasa ikichagizwa na rekodi ya kibabe iliyonayo pindi inapokuwa nyumbani kwenye Uwanja wa Taifa msimu huu.

Kati ya mabao 11 ambayo Simba imeyafunga kwenye mechi zake tisa, mabao nane imeyafungia Taifa dhidi ya timu za Prisons, Mbeya City, African Lyon na Stand United huku Kagere akinufaika zaidi kwani kati mabao matano aliyoifungia Simba hadi sasa, manne ameyapatia akicheza Dar es salaam.

Wakati Simba ikipiga hesabu za ushindi dhidi ya Alliance, vinara wa ligi hiyo Azam kesho watakuwa na kibarua cha kuvunja rekodi ya JKT Tanzania ya kutopoteza mechi watakapovaana nao kwenye Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo uliopo Mbweni jijini, huku jijini Tanga, Coastal Union wataialika Kagera Sugar.

Mechi nyingine za kesho ni kati ya Prisons na African Lyon kule Mbeya huku Ruvu Shooting ikiwa uwanja wa nyumbani, Mabatini huko Mlandizi, Pwani kucheza na Singida United.

AJIBU NAYE

Utamu wa Ligi Kuu unatarajiwa kuwa keshokutwa Alhamisi wakati Yanga itakapokuwa ugenini kukabiliana na KMC kwenye Uwanja wa Taifa jijini.

Matokeo ya wastani ya KMC kwenye Ligi Kuu msimu huu, huenda yakainufaisha Yanga ambayo pia itabebwa na uzoefu ilio nao dhidi ya wapinzani wao ambao ndio kwanza wanashiriki Ligi Kuu kwa mara ya kwanza.

Jicho la wengi litakuwa kwa kiungo mshambuliaji Ibrahim Ajibu ambaye amekuwa roho ya mafanikio ya Yanga msimu huu na hadi sasa amechangia jumla ya mabao 11 kati ya 14 yaliyofungwa na timu hiyo kwenye mechi saba ilizocheza hadi sasa.

Ajibu amefunga mabao matatu kama Heritier Makambo anayecheza wote Yanga.

Uzoefu wa kipa wa KMC, Juma Kaseja huenda ukageuka kikwazo kwa nyota wa Yanga, kupata idadi kubwa ya mabao tofauti na matarajio ya wengi ingawa bado mabeki wake wana kazi kubwa ya kufanya kuhakikisha wanaidhibiti kasi ya Yanga.

Huko Mbeya kutakuwa na shughuli pevu baina ya wenyeji Mbeya City dhidi ya Mwadui FC, wakati Ndanda FC itaikaribisha Biashara United mjini Mtwara, Stand United watakuwa nyumbani kucheza na Mtibwa Sugar, huku Mbao wataikaribisha Lipuli FC kwenye Uwanja wa CCM Kirumba.

Matokeo ya mechi hizo za kesho na Alhamisi zitatibua ramani nzima ya msimamo na mbio za ubingwa sambamba na ile ya Kiatu cha Dhahabu kwa wafungaji mabao katika ligi hiyo inayongozwa kwa sasa na Eliud Ambokile wa Mbeya City aliyepachika mabao sita.