Msuva mchezaji ghali zaidi Difaa el Jadida

Muktasari:

Msuva amejiunga na Difaa El Jadida mwaka 2017 akitokea Yanga ambayo aliitumikia kwa miaka sita.

Dar es Salaam. Mabao 13 ambayo Saimon Msuva ameyafunga kwenye Ligi ya Morocco 'Botola' na moja alilofunga kwenye Fainali za Mataifa ya Afrika (AFCON), yamempandisha chati na kumfanya awe mchezaji mwenye thamani kubwa zaidi kwenye kikosi cha Difaa el Jadida ya Morocco.

 Thamani ya Msuva imepanda hadi kiasi cha Euro 900,000 (Sh2.3 bilioni) na kumfanya awe mchezaji ghali zaidi katika kikosi cha Jadida katika kipindi hiki ambacho kumekuwa na taarifa za kuhitajika kwake na baadhi ya timu za Ulaya akitengewa dau la Euro 1.85 milioni (Sh4.8 bilioni)

Kwa mujibu wa Mtandao wa www.transfermarkt.com unajiohusisha na utoaji wa takwimu na thamani za wachezaji katika soko la usajili pamoja na thamani ya vikosi mbalimbali umeandika Difaa El Jadidia ina thamani ya euro 9.43 milioni huku Msuva thamani akiwa euro 900,000.

Ingawa mtandao huo umetaja kuwa Msuva ana thamani hiyo, taarifa kutoka Morocco zinasema kuna klabu kutoka Ulaya zipo tayari kutoa euro 1.85 milioni kuipata saini ya Msuva.

Endapo Msuva atauzwa kwa dau hilo la Euro 1.85 milioni atakuwa mchezaji ghali zaidi kuuzwa na klabu hiyo akivunja rekodi ya Hamid Ahdad na Walid Azaro waliouzwa kwa gharama ya euro 1.3 (Sh 3.4 bilioni) milioni kila mmoja.

Katika orodha ya thamani za wachezaji Difaa anayemfuatia Msuva kwa gharama ni mabeki wawili wa Morocco, Youssef Aguerdoum na Marouane Hadhoudi kila moja anathamani ya euro750, 000 (Sh 1.9 bilioni)

Mchezaji wenye thamani ndogo kabisa katika kikosi hicho ni kiungo Mmorocco Adam Lachhab thamani yake ni euro 50,000 (Sh 129 milioni).

Mtandao huo umeshindwa kuweka thamani ya Mtanzania Nickson Kibabage aliyesajili hivi karibuni na Difaa akitokea Mtibwa Sugar.