Msuva kaingia anga za Mbappe, Neymar

Muktasari:

  • Mshambuliaji huyo, alisema kuwa ametumia Dola 300 ambazo ni zaidi ya sh687,351 kama ilivyokuwa kwenye kiatu chake kilichopita ambacho kinaendana na cha sasa kwa kiasi.

HAKUNA matata kwa Sai. Siku chache baada ya kampuni ya vifaa vya michezo ya Nike kuachia viatu vipya, mshambuliaji wa Taifa Stars, Saimon Msuva mbona mapema sana ameshajimilikisha kiatu hicho ambacho kimeanza kuvaliwa na mastaa wanaotamba Ulaya.

Nike imeleta viatu vipya vinavyoitwa ‘Nike Mercurial Vapor XII Pro FG’ vyenye rangi ya kijani ya tunda kama la Apple, viatu hivyo vimejazwa udambwi- dambwi kibao, ikiwemo wepesi mguuni, pia vinaweza kusaidia kwenye kuumiliki mpira kutokana na namna vilivyotengenezwa.

Msuva ambaye yupo Morocco kwenye klabu yake ya Difaa El Jadida amekipata kiatu hicho kama kawaida yake baada ya kuagiza kutoka Hispania na unaambiwa kimeandikwa jina lake na kunakishiwa bendera ya Tanzania.

Mshambuliaji huyo, alisema kuwa ametumia Dola 300 ambazo ni zaidi ya sh687,351 kama ilivyokuwa kwenye kiatu chake kilichopita ambacho kinaendana na cha sasa kwa kiasi.

“Kuvaa vizuri imeshakuwa kama ulevi wangu vile. Napenda kuvaa viatu vya Nike ndio maana kila toleo wanalotoa nakua mwepesi kuvitafuta, hiki kipya naona kina utofauti na kile ambacho nilikichukua kipindi kile cha kombe la dunia Russia,” alisema Msuva.

Mastaa wengine ambao wameanza kuvaa toleo hilo ni Neymar na Kylian Mbappe wote wa Paris St-Germain, mastaa hao walivaa aina hiyo ya viatu kwenye mchezo uliopita wa League 1 dhidi ya Lille, Ijumaa ya wiki iliyopita.

Neymar Jr na Mbappe kila mmoja alifunga kwenye mchezo huo uliomalizika kwa PSG kuibuka na ushindi wa mabao 2-1, nyota mwingine aliyeng’ara akiwa na aina hiyo mpya ya viatu ni Dries Mertens wa Napoli aliyefunga hat trick kwenye mchezo dhidi ya Empoli kwenye Serie A.

MSUVA KUNOLEWA NA MFARANSA

Baada ya Abderrahim Talib (55) kuamua kubwaga manyanga kama Kocha Mkuu Difaa El Jadida, hatimaye klabu hiyo imemtangaza, Hubert Velud kuwa Kocha Mkuu.

Akimzungumzia mfaransa huyo, Msuva alisema ni kocha mzuri ambaye analifahamu vizuri soka la Morocco, hivyo anaweza kuwatoa hatua moja na kwenda nyingine.

Talib alibwaga manyanga kwenye klabu hiyo kutokana na kusumbuliwa na matatizo ya kiafya.