Msuva awaita mashabiki Taifa

Muktasari:

Kesho Stars inatupa kalata yake na Burundi itakayoamua kama wataendelea na mapambano ya kuwania tiketi ya kufuzu kucheza kombe la dunia, 2022 nchini Qatar, wachezaji wameomba sapoti.

YANAHESABIKA masaa Taifa Stars, kushuka dimbani na Burundi, mechi itakayoamua kama watasonga mbele ama kubaki kufuzu ya kucheza Kombe la Dunia 2022 nchini Qatar.
Straika wa timu hiyo, Simon Msuva amesema inawezekana kuwaondoa Burundi kwenye mbio za kusaka tiketi baada ya kuambulia sare ya bao 1-1 ugenini, kikubwa alichoshauri ni hamasa za mashabiki.
Msuva anaamini kwenye nguvu ya mashabiki wanapocheza nyumbani kwamba inaleta hamasa kwao, kuongeza juhudi ya kupambania taifa lao kusonga mbele kwenye michuano hiyo.
"Itakuwa mechi ngumu, lazima tujiandae bila kuwapuuza wapinzani wetu Burundi ambao wana wachezaji wenye uwezo wa juu, mbinu, kujituma na kutumia nafasi ni moja ya mambo tunayapaswa kuyafanya"
"Uwingi wa mashabiki naamini utatuongezea nguvu kuona tupo pamoja kulipambania taifa letu kusonga mbele, inawezekana kuwatoa Burundi kwa sharti la kuwaheshimu na sio kuwaogopa"
"Nimewaona namna walivyokuwa wanapambana kwenye mechi tuliocheza nao kwao sio wabaya, ila tumejipanga vilivyo kuona hatuwaangushi Watanzania,"amesema.