VIDEO: Msuva aipa ujanja Simba

Muktasari:

Saimon Msuva amesema Simba inaweza kupata matokeo mazuri ugenini katika mchezo wake na AS Vita wa Ligi ya Mabingwa Afrika, endapo itampa ulinzi mshambuliaji nyota wa timu hiyo Jean Mundele.

Dar es Salaam.Mshambuliaji wa kimataifa wa Tanzania, Saimon Msuva ameitaka Simba kuandaa ulinzi mkali kwa mshambuliaji wa AS Vita Club, Jean Marc Mundele, wakati timu hizo zitakapocheza jijini Kinshasa, Jumamosi wiki hii saa moja usiku.

Msuva ambaye timu yake Difaa El Jadidi ya Morocco iliitoa AS Vita msimu uliopita katika mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika, alisema Mundele anayevaa jezi namba 10 ni aina ya mchezaji mwenye kasi na uwezo mkubwa wa kufunga mabao hivyo anapaswa kudhibitiwa kikamilifu.s

“Huyo jamaa ni hatari sana alitufunga mabao mawili kwao DR Congo katika mchezo wa marudiano, ni mjanja sana na ndiye mchezaji aliyetusumbua kwenye michezo yote miwili.

Mabeki wa Simba wanatakiwa kumchunga, wakimuachia upenyo  anaweza kuwafunga muda wowote. Ni mzuri kumalizia mipira ya kutemwa na kipa, pia ana uwezo wa kufunga mabao ya vichwa,” alisema Msuva.

Msuva aliongeza kuwa Simba wasitarajie  watakuwa salama ikiwa mabeki watafanya uzembe wa aina yoyote mbele ya mshambuliaji huyo.

“Mundele alitufunga katika mchezo huo wa marudiano mabao mawili, lakini bahati nzuri kwenye dakika za mwisho walijisahau ndipo tuliporejesha mabao hayo mawili na kusonga mbele,” alisema Msuva.

Ingawa Mundele aliwafunga akina Msuva mabao mawili katika mechi ya marudiano ya raundi ya kwanza katika Ligi ya Mabingwa Afrika msimu uliopita, AS Vita ilitolewa na Jadidi kwa kipigo cha jumla cha mabao 3-2.

Hiyo ilifuatia sare ya mabao 2-2 ambayo AS Vita iliipata nyumbani baada ya kupokea kichapo cha bao 1-0 ugenini huko Morocco.

Kwenye mashindano hayo ambayo AS Vita iliishia raundi ya kwanza, Mundele hadi wanatolewa aliweza kupachika mabao manne katika mechi nne ambapo alifunga mabao mawili katika mechi mbili za raundi ya awali dhidi ya Mighty Wanderers ya Malawi kabla ya kuwafunga mawili Jadidi.

Kwa kudhihirisha kuwa Mundele hakubahatisha, mshambuliaji huyo alifunga jumla ya mabao 11 katika mechi 14 za Kombe la Shirikisho Afrika ambako waliangukia baada ya kutolewa katika Ligi ya Mabingwa Afrika.

Msimu huu tayari amecheza mechi tatu kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika huku akiwa amefunga mabao mawili.

Kwa ujumla katika kipindi cha misimu miwili 2018 na 2018/2019, Mundele ameitumikia AS Vita katika michezo 20 kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika na Kombe la Shirikisho Afrika ambapo amepachika jumla ya mabao 17.

Idadi kubwa ya mabao amefunga wakati AS Vita ikicheza nyumbani ambapo kwenye mechi 10 alizocheza Uwanja wa Martyrs uliopo Kinshasa unaoingiza mashabiki 80,000, Mundele amefunga mabao 12 na katika mechi 10 alizocheza ugenini amefunga matano.

Mshambuliaji huyo ambaye pia ni hatari kwa kupiga mipira ya adhabu ndogo, ana mapafu ya ‘mbwa’ na anaweza kufunga katika muda wowote wa mchezo.

Kwa kudhihirisha ubora wake, katika mabao 17 aliyofunga katika mechi 20 za mashindano ya klabu Afrika, mabao manane amefunga kipindi cha kwanza na tisa dakika 45 za kipindi cha pili.

Mbali na Mundele, Msuva pia amewashauri Simba kuwa na mbinu nyingi tofauti za kusaka bao kwa kuwa wapinzani wao wana safu imara ya ulinzi hivyo ni vigumu kuwafunga iwapo timu inatumia mbinu ya aina moja.

“Wanacheza soka la kushambulia na kujilinda siyo wepesi kufungika, tulivyocheza nao mchezo wa kwanza walikuja na mbinu za kujilinda, tuliwashambulia sana lakini walikuwa imara kwenye safu yao ya ulinzi.

Wakiwa kwao huko ndipo mambo yalipokuwa magumu kwa upande wetu cha kushukuru ni kwamba hatukuruhusu bao nyumbani hivyo tulikuwa tukicheza kwa kujiamini, walitushambulia sana na jamaa wako fiti kiukweli," aliongeza Msuva.

Wakati Mundele akifunga mabao mawili, Meddie Kagere amefunga mabao matano, Clatous Chama (manne) na Emmanuel Okwi (matatu). Mabao hayo yamepatikana na katika mechi tano ilizocheza Simba kuanzia hatua ya awali na raundi ya kwanza dhidi ya Mbabane Swallows ya Swaziland, Nkana Red Devils ya Zambia ilizocheza nyumbani na ugenini kabla ya kuvaana na JS Saoura ya Algeria.