Msuva: Sasa tutakufa na Kenya

Wednesday June 26 2019

 

By Katimu Naheka

MSHAMBULIAJI wa Taifa Stars, Simon Msuva amesema kipigo walichokipata kutoka timu ya taifa ya Senegal kilitokana na kuzidiwa uzoefu, lakini sasa wanajipanga kufanya maajabu mechi ijayo dhidi ya Kenya.

Akizungumza baada ya mchezo huo wa juzi, Msuva alisema Senegal walikuwa katika ubora mkubwa wakitumia uzoefu wao katika mashindano hayo ya Afcon.

Msuva alisema Stars kupoteza mbele ya Senegal kulitokana na kukosa uzoefu ambapo mchezo huo uliafanyika baada ya miaka 39 iliyopita tofauti na wapinzani wao ambao wamekuwa wakishiriki mara kwa mara.

Mshambuliaji huyo ambaye alitolewa kipindi cha pili na kuingia Thomas Ulimwengu, alisema baada ya matokeo hayo hivi sasa akili yao ni kusahau haraka na kujikita katika mchezo dhidi ya Kenya.

Katika mchezo ujao, Tanzania itakipiga na Kenya Juni 27, mwaka huu.

Alisema wanataka kuhakikisha wanapata pointi katika mechi mbili zijazo ambazo zitawasaidia kujipanga kwa ajili ya mashindano yajayo kama hayo.

Advertisement

“Tumepoteza dhidi ya Senegal, niseme wenzetu walituzidi kila eneo walikuwa katika ubora mkubwa, watu wanatakiwa kuelewa hii ni timu moja bora hapa Afrika tuliyokutana nayo, hatuwezi kujilinganisha na wao ingawa tulikuwa na nia ya kushinda na tulipambana,” alisema.

“Tanzania tumerudi fainali hizi baada ya miaka 39, utaona ni kipindi kirefu lakini muhimu kuangalia mechi mbili zijazo hii ilishapotea tukishinda mechi moja au zote nafikiri kuna kitu tutakuwa tumeongeza fainali zijazo.”

Advertisement