Msuva: Hasira zote sasa kwa Kenya

Muktasari:

  • Tanzania sasa inahitaji kushinda mchezo wake ujao dhidi ya Kenya ili kurudisha matumaini ya kusonga mbele katika kundi lake

Cairo, Misri. Mshambuliaji wa Taifa Stars, Simon Msuva amesema kipigo walichopokea kutoka kwa Senegal kimetokana na kuzidiwa uzoefu lakini sasa wanajipanga kwa mchezo ujao dhidi ya Kenya.

Akizungumza baada ya mchezo huo Msuva alisema Senegal walikuwa katika ubora mkubwa wakitumia uzoefu wao katika mashindano ya namna hiyo.

Msuva alisema Stars kupoteza mbele ya Senegal kumetokana na kukosa uzoefu ambapo mchezo huo unafanyika baada ya miaka 39 iliyopita tofauti na wapinzani wao ambao wamekuwa wakishiriki mara kwa mara.

Mshambuliaji huyo ambaye alitolewa kipindi cha pili na kuingia Thomas Ulimwengu alisema baada ya matokeo hayo sasa akili yao inataka kuyasahau haraka na kujikita katika mchezo dhidi ya Kenya.

Alisema wanataka kuhakikisha wanapata pointi katika mechi mbili zijazo ambazo zitawasaidia katika kujipanga katika mashindano yajayo kama hayo.

"Tumepoteza dhidi ya Senegal, niseme wenzetu walituzidi katika kila eneo walikuwa katika ubora mkubwa, watu wanatakiwa kuelewa hii ni timu moja bora hapa Afrika tuliyokutana nayo, hatuwezi kujilinganisha na wao ingawa tulikuwa na nia ya kushinda na tukapambana."