Msuli kazi : Hapa ukizubaa tu, inakula kwako!

Muktasari:

Wachezaji hao kutoka Yanga, Simba na Azam FC wanatakiwa kufanya kazi ya ziada ili kuhakikisha wanalinda nafasi zao kikosini la sivyo watajikuta wakiozea benchi.

WAKATI Ligi Kuu Bara ikitarajia kuanza mwishoni mwa mwezi huu, tayari kuna baadhi ya wachezaji wazoefu wameanza kupata matumbo joto kutokana na vita ya namba watakayokutana nayo.

Wachezaji hao kutoka Yanga, Simba na Azam FC wanatakiwa kufanya kazi ya ziada ili kuhakikisha wanalinda nafasi zao kikosini la sivyo watajikuta wakiozea benchi.

Yondani, dante V/S Moro, sonso

Beki kisiki Kelvin Yondani ‘Vidic’ pamoja na Dante wanatarajiwa kupata upinzani mkubwa kutoka kwa beki raia wa Ghana, Lamine Moro na Ally Mtoni ‘Sonso’.

Moro aliyetokea klabu ya Buildcom ya Zambia aliwahi kufanya majaribio na Simba msimu uliopita, lakini akatemwa baada ya uongozi wa klabu hiyo kudai kutoridhishwa na kiwango chake alichokionyesha katika mashindano ya Sportpesa Januari, mwaka huu.

Beki huyo ameonyesha kuwa mtulivu uwanjani na akitumia akili nyingi, hivyo kuzidi kumpa presha Yondani na Dante ambao ni mabeki wazoefu ndani ya klabu hiyo.

Pia, Yondani anakabiliwa na ushindani mwingine kutoka kwa Sonso aliyesajiliwa msimu huu akitokea Lipuli FC ya Iringa.

Sonso alicheza vizuri pamoja na Moro katika mchezo wa hatua ya awali ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Township Rollers ya Botswana uliofanyika Agosti 10, kwenye Uwanja wa Taifa.

Juma Abdul V/S Paul Godfrey’Boxer’/Ali Ali

Beki wa kulia wa Yanga, Juma Abdul anatarajia kuendelea kupata upinzani kutoka kwa Paul Godfrey ambaye msimu uliopita alicheza karibu mechi zote za Yanga.

Abdul ameshindwa kuitetea namba yake mbele ya Boxer na hata msimu huu hali inaweza kuendelea kuwa hivyo kutokana na kiwango bora anachozidi kukionyesha beki huyo chipukizi.

Pia, hivi sasa Yanga imesajili beki mwingine, Ali Ali, kutoka KMC ambaye naye anazidi kuiweka nafasi ya Abdul reheni msimu ujao.

Abdul ni mmoja wa mabeki wa pembeni mahiri nchini, lakini majeruha ya mara kwa mara yamekuwa yakiathiri kiwango chake.

Feisal Salum V/s Mapinduzi Balama/Mohammed Issa Banka

Moja ya viungo wenye udambwidambwi uwanjani (fundi) ni Feisal Salum ‘Fei Toto’ na kutokana na soka lake maridadi amekuwa kipenzi cha mashabiki wa Yanga.

Hata hivyo, ujio wa Mapinduzi Balama kutoka Alliance FC unaweza kuwa kikwazo kwa Fei Toto kupata namba katika kikosi cha kwanza msimu ujao.

Mapinduzi ameonekana kuwavutia mashabiki wa Yanga kwa muda mfupi tu kutokana na kiwango chake, na zaidi alivyocheza kwa ubora mkubwa katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Township Rollers ya Botswana, wiki iliyopita, kwani alikuwa injini ya timu hiyo katikati ya uwanja.

Pia, Fei Toto anakabiliwa na ushindani mwingine kutoka kwa Mohammed Issa ‘Banka’ ambaye ni kama amerejea upya baada ya msimu uliopita kutoitumikia timu hiyo kwa muda mrefu kutokana na kufungiwa kwa miezi 14 na Kamati ya Kuzuia na Kupambana na Dawa zisizoruhusiwa michezoni ya Kanda ya Tano Afrika (Rado), baada ya kukutwa na hatia ya kutumia bangi.

Banka amerudi kwa kishindo kwa kuonyesha soka la kiwango cha juu na ufundi mkubwa, hivyo kuzidi kutishia nafasi ya Fei Toto kikosini.

Jonas Mkude V/s Sharaf Shiboub

Baada ya kuondoka kwa James Kotei, mashabiki wengi wa Simba waliamini Jonas Mkude atakuwa hana mpinzani katika kikosi cha kwanza cha kocha Patrick Aussems, lakini kumbe ni tofauti.

Ujio wa kiungo mrefu, mwenye mwili mkubwa na mweusi Sharaf Shiboub kutoka klabu ya Al Hilal ya Sudan utamfanya Mkude kukomaa na kupigania nafasi yake kikosini.

Shiboub ameonyesha kuwa yeye ni mtu wa kazi na mashabiki tayari wamemkubali na huwaambii kitu jambo ambalo linazidi kumuweka Mkude katika wakati mgumu.

Manula V/S Kakolanya

Nafasi nyingine itakayoibua ushindani wa namba ndani ya kikosi cha Simba ni golikipa.

Awali, Aishi Manula ndiye alikuwa panga pangua katika kikosi hicho lazima acheze langoni, lakini ujio wa Beno Kakolanya unaweza ukawa kengele kwa kipa huyo kutoka Morogoro kuwa lazima ajipange. Hakuna mtu asiyeufahamu ubora wa Kokalanya akiwa langoni kwani licha kukaa nje ya dimba kwa muda kutokana na kuwa na mgogoro na timu yake ya zamani, Yanga, lakini bado ni miongoni mwa makipa bora hapa nchini, hivyo Manula anapaswa kujipangwa hasa.

Kutokana na mtifuano wa kugombea namba katika vilabu hivyo, mafanikio yataonekana uwanjani msimu huu.