Msimchezee Tambwe nyie!

Tuesday January 8 2019

 

By Olipa Assa

SAWA msimu uliopita aliumaliza bila kufunga bao katika Ligi Kuu, lakini straika Amissi Tambwe sio mtu wa mchezaji na wapinzani wake hawapaswi kumchezea hata kidogo kwa namna alivyofunika mwanzo mwisho nchini.

Straika huyo kutoka Burundi, ndiye anayeonekana mchezaji aliyeziwezea Simba na Yanga, tofauti na wachezaji wengine waliwahi kuzihama timu hizo kwenda upande mmoja kama ilivyomkuta Haruna Niyonzima.

Tambwe alijiunga na Yanga mwaka 2014 akitokea Simba akitoka kuwa Mfungaji Bora akimaliza na mabao 19 na ile kutua tu Jangwani alimaliza wa pili nyuma ya Saimon Msuva aliyempokea Kiatu cha Dhahabu akiwa na mabao 17 dhidi ya 14 aliyokuwa nayo.

Straika huyo alijiunga Simba mwaka 2013 akitokea Vital’O ya Burundi akitoka kuwapa taji la michuano ya Kagame, huku yeye akiwa Mfungaji Bora.

Kung’ara kwa Tambwe na kumfunika hadi Niyonzima ambaye alijiunga Simba akitokea Yanga msimu uliopita na kuwa na mafanikio madogo, kumewaibua wadau kadhaa kumchambua na kusisitiza Mrundi huyo ni kiboko.

Kama hujui tu ni kwamba Tambwe tangu atue nchini amefunga jumla ya mabao 70 katika Ligi Kuu, mbali na mengine ya mechi za kimataifa, Kombe la Mapinduzi, Kombe la FA ama michezo ya kirafiki na kuwafunika nyota wote wa kigeni.

Hata hivyo, ishu yake ya kung’ara zaidi ya Niyonzima aliyekuwa mfalme Yanga na kupotea Msimbazi, Kocha wa Coastal Union, Juma Mgunda alisema; “Kwa namna Tambwe alivyoondoka Simba kwenda ni kama anaanza moja, akiwa na tahadhari ya kutunza kiwango chake ili kuepuka kuzomewa hilo limemsaidia kumjenga na kumudu kucheza kwa kiwango cha juu, tofauti na ilivyokuwa kwa Niyonzima.”

Naye kiungo wa zamani wa Simba na Yanga, Mohammed Banka alidai kilichombeba Tambwe ni kule kupambana ili kuwaonyesha waliomtema kizengwe, lakini alisema nyota wa kigeni anapokaa kwa muda mrefu kwenye timu za watani hawapaswi kuhamahama zaidi ya kuondoka kabisa nchini.

“Mfano mzuri ni pale Emmanuel Okwi alipoenda Yanga, hakuwa na wakati mzuri sana kama alivyokuwa Simba, Niyonzima hakustahili kutua Msimbazi alitakiwa aende nje ya nchi tofauti na Tambwe aliyetemwa na kunyakuliwa Yanga na kufanya kweli,” alisema.

Kiraka wa zamani wa klabu hizo, Nurdin Bakari alitoboa siri ya Tambwe kujiwekea ufalme ndani ya timu hizo mbili kuwa aliondoka kama yatima Msimbazi.

“Simba walimuacha kwa dharau Tambwe akiwa ametoka kufunga mabao 19 hiyo ilimfanya asijione staa wa kurembaremba zaidi ya kujituma, hilo lilimkuta pia Kelvin Yondani alipoachana na Simba kutua Yanga, ishu zao ni tofauti na Niyonzima.”

Advertisement