Msimbazi mjipange, hao Singida wamepania!

Muktasari:

  • Minziro ameliambia Mwanaspoti, Singida imejipanga kupambana ili kutogeuzwa ngazi ya kuipa Simba taji la pili mfululizo katika ligi hiyo kwenye uwanja wao wa nyumbani.

SINGIDA.SIMBA mjipange aisee, kwani wapinzani wenu wa Singida United wamejipanga kuwatibulia kesho Jumanne kwenye Uwanja wa Namfua, mjini hapa.

Unaambiwa mipango iliyosukwa na Kocha Fred Felix ‘Minziro’ kuelekea mchezo huo wa Ligi Kuu Bara, kama Simba haitajipanga vizuri,itaumbuka kweupee!

Minziro ameliambia Mwanaspoti, Singida imejipanga kupambana ili kutogeuzwa ngazi ya kuipa Simba taji la pili mfululizo katika ligi hiyo kwenye uwanja wao wa nyumbani.

Simba ambayo jana ilikuwa Uwanja wa Uhuru kuvaana na Ndanda, itaifuata Singida asubuhi ya leo ili kuumana nao kesho Jumanne kabla ya kugeuza fasta kuwahi pambano lao la kimataifa la kirafiki dhidi ya Sevilla ya Hispania litakalopigwa Alhamisi pale Taifa.

Kocha Minziro alisema hataki kuona Simba inatangazwa bingwa Namfua, hivyo amewaandaa vijana wake kupambana kiume na kuondoka alama tatu akiamini Simba itakuwa na uchovu.

Lakini Simba baada ya kusikia tambo hizo za wenyeji wao wametuma salamu fupi kwa kuwataka wachezaji, mashabiki na viongozi wa Singida United, wajiandae kisaikolojia tu, kwani kesho jioni watatangaza ubingwa.

“Wachezaji wangu wapo vizuri na wana kiu ya ushindi dhidi ya Simba. Niwaombe tu mashabiki wetu waje kwa wingi uwanjani waishangilie timu yao mwanzo mwisho. Kwani nina uhakika kitaeleweka, kwa jinsi tulivyojiandaa,” alisema Minziro kwa kujiamini.

Hata hivyo, mashabiki wa Simba na Singida wametambiana kuelekea mchezo huo wa kesho ambapo, Lameck Longino shabiki wa Simba kutoka Isamilo, Mwanza alisema Simba ilizoa pointi tisa Kanda ya Ziwa, hivyo haiwezi kushindwa kuitungua Singida kwao.

Naye shabiki wa Singida, Haji Kilimbida, alijibu mapigo kwa kudai kama Mkurugenzi wa Singida Festo Sanga atahudhuria mchezo huo, basi atarajie upinzani mkubwa kwani yeye na wenzake wameshindwa kuitangaza mechi hiyo muhimu kwa ajili ya kupata mapato mazuri ambayo yangewasaidia kupunguza madeni yao.

Hata hivyo, Ofisa Habari wa Singida, Karesi Katemana, alikiri kutokuitangaza mechi hiyo na kudai bado hawajachelewa.

“Hao wanaolalamika, ni watu wa ajabu. Mechi hii ipo kwenye ratiba ya TFF tangu Agosti mwaka jana.