Msimbazi mbona freshi, Alliance wabishi

Muktasari:

  • Mwanaspoti ambalo lilikuwepo mwanzo mwisho katika mchezo huo inakuletea mambo mbalimbali yaliyojiri, ambayo haikuwa rahisi kwa mashabiki kuyaona kwa jicho la kawaida.

MWANZA.SIMBA hawataki mchezo kabisa kwenye mbio za kutetea ubingwa wake. Juzi mashabiki wake walikuwa na presha kubwa kwenye mchezo huo dhidi ya Alliance, ambapo waliingia uwanjani wakiwa wanyonge.

Hata hivyo, mwisho wa mchezo hawakuwa wanyonge kama ilivyokuwa dhidi ya Kagera Sugar kule Kaitaba, ambako walichapwa mabao 2-1.

Katika mchezo huo uliopigwa Uwanja wa CCM Kirumba, Simba ilichomoza na ushindi wa mabao 2-0 na kurejesha shangwe uwanjani.

Lakini, haikuwa kazi rahisi kwa Simba kuondoka na ushindi katika mpambano huo kwani, walikutana na upinzani mkali kutoka kwa Alliance ambao, nao walicheza soka la kuvutia.

Mwanaspoti ambalo lilikuwepo mwanzo mwisho katika mchezo huo inakuletea mambo mbalimbali yaliyojiri, ambayo haikuwa rahisi kwa mashabiki kuyaona kwa jicho la kawaida.

SIMBA WAPITIA NJIA YA YANGA KIRUMBA

Iko hivi Yanga katika mechi zake walizocheza hapa Mwanza wakati wakiingia kupasha wakipita pembeni mwa uwanja kisha kuingia uwanjani tofauti na timu nyingine ambazo huingia moja kwa moja.

Lakini, juzi Simba nao waliingia na staili hiyo ambapo walipita pembeni mwa mstari wa uwanjani na kuzunguka mpaka kwenye kibendera cha kupigia kona na kuingia uwanjani.

Alliance wao waliingia kama kawaida uwanjani kupasha bila ya mbwembwe zozote huku wakilindwa na makomandoo.

MAKOMANDOO YANGA WATIA TIMU

Wale mashabiki na wanachama wa Yanga ambao timu hiyo inapokuja jijini Mwanza hufanya kazi ya ulinzi, juzi walionekana wakiwa bize kuhakikisha mambo ya ulinzi yanakwenda sawa kwa Alliance.

Muda wote makomandoo hao wa jijini hapa walikuwa wakiendesha ulinzi huo jambo ambalo liliwastua wengi waliofika uwanjani hapo wakijiuliza wamefuata nini.

Hata hivyo, makomandoo wa Simba nao walikuwa makini kuhakikisha mambo yanakwenda vyema pasipo kuwepo kwa hujuma yoyote kwa timu yao.

BAO LA KIDEO LA NIYONZIMA

Kiungo fundi wa mpira, Haruna Niyonzima juzi aliwaduwaza mashabiki baada ya kufunga bao la kideo lililoamsha shangwe uwanjani hapo. Niyonzima alipokea krosi safi ya Mzamiru Yassin kisha akamtoka Beki Siraji Juma na kupiga shuti lililomwacha kipa John Mwanda akishangaa.

Hilo lilikuwa bao lake la kwanza katika uwanja wa Kirumba akiwa na Simba.

SHABIKI WA ALLIANCE AWAFUNIKA SIMBA

Alliance wana shabiki mmoja maarufu sana, Kisonzo Kisonzo ambaye kama ukimwendekeza kusikiliza shombo zake basi unaweza kujikuta dakika zote 90 unamwangilia yeye tu. Juzi shabiki huyo alikuwa kivutio uwanjani hapo kwa staili yake ya kushangilia huku akitoa kauli za shombo.

Lakini, baada ya dakika 90 za mchezo hakujulikana aliondoka vipi uwanjani hapo. Hakuaga kabisa.

AUSSEMS AFUNGUKA

Patrick Aussems amesema mchezo ulikuwa mgumu hasa kipindi cha kwanza, lakini amepata nguvu baada ya ushindi huo. Alisema kwa sasa amekuwa akipanga kikosi tofauti ili kuwapa mapumziko wachezaji wake kutokana na mechi nyingi.

“Angalia keshokutwa (leo)tunacheza na KMC hivyo ni muhimu kupanga kikosi tofauti kwani, ukiangalia tunapumzika siku moja moja tu hivyo ni muhimu kubadilisha kikosi kila mara,” alisema Aussems.

KOCHA ALLIANCE ATEMA CHECHE

Kocha Msaidizi wa Alliance, Kessy Mziray alisema mchezo huo ulikuwa rahisi kwao na wangeondoka na ushindi iwapo tu washambuliaji wao wangekuwa makini.

Alisema Simba hawakutengeneza nafasi nyingi za kufunga kama wao, lakini wakatumia chache walizopata kupata mabao hayo mawili yaliyomaliza mchezo huo mapema tu.

“Tujilaumu wenyewe kwenye huu mchezo kwani, tungekuwa makini basi tungeondoka na pointi tatu kwa sababu tulikosa mabao mengi ya wazi,” alisema Mziray.

Ushindi huo wa juzi umewafanya Simba kufikisha pointi 63 huku Alliance wakibaki na alama zao 37.