Msikie Dullah Mbabe anachomwambia Cheka

Monday December 10 2018

 

By Imani Makongoro

WAKATI mashabiki wa ndondi nchini wakihesabu siku tu ili kumaliza ubishi wa nani mkali kati ya Abdallagh Pazi (Dullah Mbabe) na Francis Cheka, Mbabe ameibuka na ujumbe mzito kwa Cheka unaambiwa.

Iko hivi, Dullah Mbabe na Cheka watapanda ulingoni Desemba 26 kwenye Ukumbi wa PTA, Sabasaba jijini Dar es Salaam kuzichapa kuwania mkanda wa ubingwa wa Mabara wa WBF.

Pambano hilo la uzani wa Super Middle Kg 76 la raundi 12 limeteka hisia za mashabiki wa ndondi nchini ambao baadhi wanaamini ‘ufalme’ wa Cheka kwenye ndondi unaelekea ukingoni huku wengine wakiamini, Dullah Mbabe ameingia anga za ‘kifo’ kukubali kuzichapa na Cheka.

Wakati tambo za mashabiki wa mabondia hao zikiendelea, Dullah Mbabe ameibuka na kutamka pambano lake na Cheka ni sawa na mbuzi kudondokea kwenye himaya ya fisi.

“Bila shaka kitakachompata mbuzi kila mmoja anakielewa, hivyo Cheka ajiandae,” alisema Dullah Mbabe na kuendelea.

“Anaweza kudhani labda uzoefu alionao unaweza kumbeba kwenye pambano letu, lakini nimwambie tu ngumi hazina uzoefu, kama anabisha akamuulize, Wladimir Klitschko kwa Anthony Joshua (Wladimir bingwa wa zamani wa uzani wa juu aliyepigwa na Joshua).”

Mbame alisema amejiandaa kwa ushindi, hana hofu wala presha ya pambano hilo.

Advertisement