Mshindo awashangaa wanaozusha Rostam amwaga fedha Yanga

Muktasari:

  • Akizungumza na Mwanaspoti, Msola alisema kumekuwa na taarifa ambazo hazina ukweli ambazo amezichukulia kama kukwamisha zoezi lao la kuchangisha fedha kutoka kwa wanachama baada ya baadhi ya watu wasiokuwa na nia nzuri na klabu hiyo kuzusha taarifa za kupatikana kwa muwekezaji.

MWENYEKITI wa klabu ya Yanga, Mshindo Msola amekanusha vikali suala la Rostam Azizi kuwekeza katika klabu yao na kuwaomba wanachama wa klabu hiyo kupuuza uvumi huo na kuendelea kuichangia klabu yao.

Akizungumza na Mwanaspoti, Msola alisema kumekuwa na taarifa ambazo hazina ukweli ambazo amezichukulia kama kukwamisha zoezi lao la kuchangisha fedha kutoka kwa wanachama baada ya baadhi ya watu wasiokuwa na nia nzuri na klabu hiyo kuzusha taarifa za kupatikana kwa muwekezaji.

Alisema suala hilo halipo na halijafanyika popote ni maneno ya watu wasiokuwa na nia nzuri na klabu yao na kuendelea kuwaomba wanachama wao kuendeleza zoezi lao la kuichangia timu hiyo ili iweze kufikia malengo ya kupata kiasi cha fedha ambazo zitaweza kuisaidia timu kusajili kikosi kizuri.

"Hakuna mkataba wowote ambao klabu imeingia na muwekezaji wa aina yeyote ni uzushi bado tunaendelea na mchakato wa kuchangishana na ikitokea tumepata tutatoa taarifa sasa tunaomba wanachama wetu waendelee na mchakato uliopo wa kuichangia klabu,"

"Zoezi la kuchangishana lipo miaka yote utofauti uliopo sasa ni namna ambavyo tumekuwa tukichangishana na tutaendelea kufanya hivyop kila pale klabu itakapokwama tutawatumia wanachama wetu kuwaomba wachangie pale tulipokwama," alisema Msola.