Mshambuliaji Taifa Stars aaga Kenya kwa majonzi

Monday November 20 2017

 

By ELIYA SOLOMON

PAZIA la Ligi Kuu Kenya, limefungwa kwa majonzi na winga wa Kitanzania, Abdul Hilal baada ya timu yake ya Tusker kuambulia kipigo cha mabao 4-0 ugenini dhidi ya Ulinzi Stars.

“Wiki ijayo narudi nyumbani kujiunga na Kilimanjaro Stars, lakini sina furaha kwani huku ligi imemalizika vibaya, sikutegemea kama tungefungwa mabao yote hayo.

“Tayari Gor Mahia ni bingwa hatukuwa na ambacho tunakipigania, siwezi kushangaa sana,” alisema Hilal, winga huyo ambaye ameitwa kwenye kikosi cha Kili pamoja na Abdallah Hamis wote wakitokea Ligi Kuu ya Kenya, KPL.

Kipigo hicho kitakatifu kimeifanya timu hiyo kumaliza ligi kwenye nafasi ya sita ambayo ni mbaya kwao kwa kuwa ndio walikuwa mabingwa watetezi.

Kwa upande mwingine, Abdallah Hamis na Sony Sugar yake walifunga pazia la KPL kwa sare ya mabao 2-2 na mabingwa wa ligi hiyo Gor Mahia, inayofundishwa na kocha wa zamani wa Simba, Dylan Kerry.