Mseja bana, mshahara Simba, tizi Makurumla

Sunday September 9 2018

 

By DORIS MALIYAGA

AKIWA hana namba wala nafasi ya kucheza katika kikosi cha Simba, Kipa Emmanuel Mseja ameamua kuendelea kujifua mazoezi peke yake Uwanja wa Makurumla jijini Dar es Salaam, huku akiendelea kupokea mshahara wake Msimbazi.

Mseja ni miongoni mwa wachezaji ambao wamesajiliwa Simba na analipwa mshahara wake kama kawaida lakini ni kama hayuko kwenye programu ya kocha, Mbelgiji Patrick Aussems.

Kipa huyo aliyesajiliwa msimu uliopita akitokea Mbao FC ya Mwanza pamoja na kipa mwingine, Said Mohamed ‘Nduda’, japo mwenzake amejiunga na kikosi hicho wiki iliyopita baada ya kupewa taarifa ya kufanya hivyo, huku yeye akikaushiwa.

Akizungumza na Mwanaspoti, Mseja alisema; “Mimi ni mchezaji wa Simba kwa sababu nimesajiliwa na nalipwa mshahara kama kawaida, lakini ndiyo hivyo, nipo nipo tu. Sijapewa taarifa ya kujiunga na timu na siwezi kufanya uamuzi wangu tu kwenda mpaka watakaponiambia hivyo imenibidi niendelee kujifua kivyangu.”

“Nafanya mazoezi na makipa wenzangu katika Uwanja wa Makurumla ili kujiweka fiti, wakati wowote Simba wakiniambia kuwa wananihitaji kwenye timu nitafika,” alifafanua kipa huyo ambaye pamoja na kuwepo kikosi cha msimu uliopita, lakini hakucheza mechi hata moja ya Ligi Kuu Bara.

Kipa huyo pia aliachwa kwenye ziara ya Simba nchini Uturuki ilipoenda kuweka kambi na hakutambulishwa kwenye Simba Day kama mmoja ya wachezaji wa msimu huu.

Advertisement