Msala, Kuna mtu anavua jezi namba 10 Yanga

Friday October 16 2020

By KHATIMU NAHEKA

TOLEO la jana Alhamisi tuliona jinsi mshambuliaji mpya wa Yanga, Said Ntibazonkiza maarufu kama Saido akielezea kwamba, bado ni mchezaji mwenye uwezo na wanaombeza watajua ubora wake uwanjani na sasa anaendelea kuelezea mambo mbalimbali akianza na kuelezea mchezo wa Taifa Stars dhidi ya Burundi ulivyokuwa.

VITA YAKE NA MKUDE

Kwenye mchezo dhidi ya Stars, Ntibazonkiza ndiye aliyefunga bao pekee la ushindi lakini kabla alitokea kukwaruzana na kiungo mzawa, Jonas Mkude na kumtengenezea kadi ya pili ya njano iliyozaa nyekundu sasa jamaa anaelezea mkasa mzima.

“Kwa kiasi fulani nilidhamiria kumtengenezea ile kadi ya pili ya njano unafahamu ukiwa uwanjani kuna wakati ari tofauti. Nakumbuka mimi ndio nilitangulia kumfanyia kosa wakati fulani nikamuomba msamaha akaelewa inatokea katika mpira unajua tena yeye anacheza nafasi ya kiungo mimi nacheza mbele. Lakini, baadaye nikaona kama amekasirika nikawa nimeshajiandaa kukutana naye tena nikitambua tayari alikuwa na kadi ya kwanza ya njano ambayo nayo nilimtengenezea alipoushika mpira.

“Kuna wakati niliposhika mpira akaja kwa hasira kama kulipiza ni kweli aliniumiza kidogo na ilikuwa ni adhabu ya kweli na mwamuzi aliiona. Baada ya hapo nikaona kama ana jazba nikasema hapa hapa ndio nitamuongezea hasira na kweli akafanya hivyo nadhani alishasahau kuwa ana kadi ya kwanza ya njano.

“Mwamuzi akanipa kadi ya njano lakini pia ndio likatokea lile lililotokea kwa kupewa kadi nyekundu. Kwangu ilikuwa ni faida kwa timu yangu na kama uliona baada ya hapo tulipata nafasi ya kuishambulia zaidi Tanzania wakati wakijaribu kujipanga na tukapata lile bao muhimu na tukashinda mchezo ule.

Advertisement

“Sidhani kama atakuwa na akili hiyo ya kutaka kulipiza lakini wala siogopi kwanza mimi ndio napenda vitu vya namna hiyo kwani ushindani kwa timu yangu na timu pinzani hasa watani wa jadi nitakuwa makini sana kwa kuwa tayari nimeshamjua kupitia mchezo huu wa kwanza tuliokutana tutapambana.

Akiwa katika mchezo dhidi ya Stars kumbe aliukubali sana uwezo wa beki wa Stars na klabu yake ya Yanga, Bakari Mwamnyeto kwa namna alivyoonyesha utulivu ingawa hakujua na hapa anamuelezea.

“Nilikuwa sijui kama ni beki wa Yanga, lakini katika mchezo ule aliongoza vizuri safu ya ulinzi alikuwa na utulivu mkubwa. Unajua kipindi cha kwanza mfumo wetu haukuturuhusu kushambulia angalau kipindi cha pili na kuna wakati tulilazimika kutumia akili, lakini bado alikuwa imara nafikiri Yanga imepata beki mzuri sio yeye tu hata yule aliyecheza kwenye kiungo (Feisal Salum) naye nimeambiwa ni beki wa Yanga ni mzuri alionyesha kiwango kizuri.”

MIPANGO YAKE YANGA

“Napenda kazi yangu ndio izungumze kuna wakati unaweza kuongea sana, lakini baadaye ukajikuta uwanjani hakuna kitu. Klabu hii inataka mafanikio na nimeambiwa kwa miaka mitatu hawajapata makombe utaona kazi iliyopo hapa ndio maana nimeamua haraka nikimaliza majukumu ya timu ya taifa nitarudi hapa kuungana na wenzangu ili kuzoea. Nataka kushinda mataji hapa ili niache alama lakini kikubwa ni ushirikiano baina yetu na wachezaji na viongozi na mashabiki wetu kuwa pamoja na sisi.”

WACHEZAJI WARUNDI

“Kuna tofauti mbili kubwa za kucheza mpira kati ya Burundi na Tanzania, Burundi tupo vizuri sana kiufundi na Tanzania wanapenda sana kutumia nguvu zaidi kuliko ufundi ndio maana ukiwalinganisha watu wawili yule mwenye ufundi anaonekana yuko vizuri zaidi kuliko anayetumia nguvu.

“Unajua mtu ambaye anatumia ufundi zaidi anaweza akapata nafasi ya kuongeza nguvu na akafanikiwa kwa kuwa nguvu pia zinahitajika. Lakini, yule mwenye nguvu wakati mwingine ni vigumu kuongeza ufundi, sina maana kwamba wachezaji wote Watanzania wako hivyo ila wengi wanapenda kutumia nguvu na pia wenye ufundi pia wapo tunachochukulia hapa ni kwa ujumla wake ndio maana wachezaji wengi wa Burundi wana miili midogo midogo, lakini ufundi ni mwingi sana uwanjani.

“Unajua nina timu ya watoto kule Burundi, watu wengi wanapenda kuelekeza akili zao katika timu za wakubwa shida hatuwazi kuhusu kuanza kuwaandaa wachezaji wakiwa wadogo. Sijui kwa Tanzania kama kuna mfumo mzuri wa kulea watoto wakiwa wadogo.

“Afrika Mashariki nzima inatakiwa kuwa na lugha moja katika hili kama kweli wanataka kuwa bora na kuzalisha wachezaji bora.”

BEKI SIMBA AMPIGIA

Said wakati akizungumza na Mwanaspoti alikuwa akiwasiliana na beki wa Simba, Erasto Nyoni na wakazungumza mambo kibao na akamueleza jinsi Tanzania ilivyo kwa maana ya Simba na Yanga.

Kumbe jamaa wanajuana tangu wakiwa Arusha katika kituo cha Rolling Stone ambayo imekuwa ikifanya kazi ya kulea wachezaji kwa miaka mingi na sasa anaelezea.

“Unajua nimeanza kucheza mpira nikiwa mdogo sana nafikiri watu wa Arusha ukiwauliza kuhusu mimi wengi wananijua. Sikuanzia njiani sababu kubwa ni kwamba, baba yangu alikuwa mchezaji na hata sasa bado anacheza mpira wa uzeeni. Najuana sana na Erasto Nyoni tulikuwa naye kule na hata sasa hapa uliponikuta nilikuwa nafanya naye mawasiliano, amenikumbusha mbali alinitumia picha yangu ya utotoni kabisa nikiwa nimeshinda kombe. Nakumbuka mbali sana kwa hiyo bahati nzuri kwangu pia hata Ulaya nilienda nikiwa mdogo ndio maana nimekaa miaka mingi kule.”

JEZI YA YACOUBA

Said huenda akawashtua Yanga kwani anataka kutumia jezi namba 10 ambayo inavaliwa na mshambuliaji mpya Yacouba Sogne na jamaa anasisitiza akiikosa hiyo anaweza kucheza akiwa hana furaha.

“Napenda kutumia jezi namba 10 hii ni namba ninayoipenda na nimeitumia karibu klabu zote nilizocheza huwa naona kama nimezaliwa kutumia jezi hii hivyo, unaponiambia hapa Yanga ina mtu naona kama nachanganyikiwa. Nitazungumza na uongozi na anayeitumia ili anipatie.

“Nitamuomba anipatie, nilianzisha biashara ya tisheti zangu maalum kama sehemu ya kujiingizia kipato lakini jinsi zilivyotengenezwa nembo yake kuna namba 10 pia ndio maana nakwambia hivyo, acha tuone kipi uongozi watanisaidia katika hili.

NJE YA SOKA

“Kwa sasa mimi sio mchezaji mdogo nashukuru Mungu nimefanya uwekezaji katika maeneo mengi ambayo yaniingizia kipato cha uhakika.

“Nilipokuwa Uholanzi nilisomea Biashara ya Kimataifa niliona nifanye hivyo kwani kuna maisha baada ya soka sasa elimu hiyo ndio inanisaidia lakini pia nafurahi kuona katika kibiashara nawasaidia wengine kupata ajira hilo linanipa faraja kwamba, kile nilichopata pia kinawasaidia wengine na familia zao.

FAMILIA

“Sipendi sana kuelezea maisha yangu ya kifamilia lakini nimeoa na nina watoto tena nina watoto wengi (anacheka) nashukuru Mungu maisha yanaendelea hakuna shida na kwa kuwa mimi ni Muislam usishangae nikaoa wake wengi zaidi.”

Advertisement