Mrithi wa Djuma Simba huyu hapa

Muktasari:

Kocha Mkuu wa Simba Patrick Aussems, ametaja sifa nne za msaidizi wake anayemtaka katika kikosi hicho, kujaza nafasi ya Mrundi Masoud Djuma.

Dar es Salaam. Muda mfupi baada ya Masoud Djuma kupanda ndege kurejea nyumbani kwao Burundi, Kocha Mkuu wa Simba, ametaja sifa nne za msaidizi wake anayemtaka katika kikosi hicho.

Djuma aliondoka jana alfajiri kurejea Burundi baada ya Simba kusitisha mkataba wake kwa madai ya kutokuwa na uhusiano mzuri na Aussems raia wa Ubelgiji.

Akizungumza na gazeti hili Dar es Salaam jana, Aussems alisema sifa ya kwanza anahitaji kocha msaidizi mzawa anayetoka nchini ambaye atamuachia urithi wake atakapoondoka nchini.

Aussems aliyejiunga na Simba kujaza nafasi ya Mfaransa Pierre Lechantre, alitaja sifa ya tatu anataka msaidizi mwenye malengo ambaye atafanya kazi weledi.

Kocha huyo alisema anataka kocha mwenye nidhamu ambaye atafanya kazi vyema kwa kufuata maelekezo yake na siyo vinginevyo.

Aussems alisema katika nchi zote alizofanya kazi, alifanya kazi na msaidizi namba moja anayetoka katika nchi husika, hivyo anataka kuendeleza falsafa hiyo akiwa Simba.

"Nahitaji msaidizi baada ya kuondoka Djuma,unajua kila nchi niliyokuwa naenda kufanya kazi nilikuwa nahitaji msaidizi kutoka ninayofanyia kazi

"Lengo langu kama nitaondoka kuna kitu cha faida naacha kwa kocha aliyekuwa anafanya kazi na mimi. Nina Mohammed (Mwarami) ambaye ni kocha wa makipa na Adel (Erane) anafanya kazi ya mazoezi ya viungo nina furaha kufanya nao kazi lakini nigependa kumuongeza mmoja,” aliongeza Aussems.

Alisema hana mpango wa kuongeza kocha wa kigeni kwa kuwa ana amini Tanzania ina makocha wazuri ambao watakuwa msaada kwake katika kutekeleza majukumu yake Simba.

Hata hivyo, alionya hataki kocha msaidizi wa kuchaguliwa na uongozi na atakuwa tayari kubwaga manyanga endapo vigogo wa Simba wataingilia mchakato huo.

Aussems alidokeza ameagiza kwa uongozi atafutiwe makocha watatu ambao atawafanyia usajili kwa kuangalia vigezo stahiki anavyotaka kabla ya kumteua mmoja atakayemrithi Djuma.

Akizungumzia uwezekano wa kumchukua kocha wa Mbao Amri Said ‘Stam’, Aussems alisema hafahamu kama atakuwa mmoja wa makocha watatu watakaoingia katika usaili huo.

Mbali na Amri ambaye amewahi kucheza Simba na kuinoa Lipuli kabla ya kutua Mbao, nahodha wa zamani wa timu hiyo Selemani Matola anapewa nafasi ya kurithi mikoba ya Djuma.

Akizungumza kwa simu jana, kocha huyo wa Lipuli alisema hana taarifa za kutakiwa na Simba na hakuna kiongozi wa klabu hiyo aliyefanya naye mazungumzo.

“Sina taarifa kama Simba wananitaka, lakini kama wananihitaji mimi kwa sasa ni kocha wa Lipuli kwa hiyo kuna vipengele vya mkataba vinanibana itabadi viangaliwe,” alisema Matola.

Katika hatua nyingine, Ausseims alisita kuweka bayana mzozo wake na Djuma ingawa alidai Mrundi huyo kocha mzuri mwenye uwezo wa kufundisha soka.