Mpenja : Sikia alipokutana na Makambo ,Kagere-3

Muktasari:

  • KATIKA sehemu mbili zilizopita za mahojiano haya na Baraka Mpenja, mtangazaji huyo wa mechi za soka kwenye Azam TV alieleza kuhusu mikasa yake ya kimapenzi na usaliti ulivyomsukuma hadi kuoa haraka na kutumia usafiri wa bodaboda yeye na bi harusi wake mpya aliyekuwa ndani ya shela wakipanda mshikaki wakitokea kanisani kuoana. Sasa endelea...

KATIKA sehemu mbili zilizopita za mahojiano haya na Baraka Mpenja, mtangazaji huyo wa mechi za soka kwenye Azam TV alieleza kuhusu mikasa yake ya kimapenzi na usaliti ulivyomsukuma hadi kuoa haraka na kutumia usafiri wa bodaboda yeye na bi harusi wake mpya aliyekuwa ndani ya shela wakipanda mshikaki wakitokea kanisani kuoana. Sasa endelea...

MISEMO INAVYOMPA ULAJI

Wakati wengine wakiumizwa na misemo hiyo kutokana na kuwapa maumivu pale timu zao zinapofungwa, unaambiwa mtangazaji huyo huwa anajiingizia kipato kutoka kwa mashabiki wa timu hiyo na anaweka wazi kila akitangaza vizuri mabao ya Yanga anatuzwa na kuchukiwa na Simba na kwa upande wa pili ni hivyo hivyo.

Huwa sipendi kujitangaza sana mitandaoni kama nimepata chochote, ila ukweli misemo hiyo imenipa umaarufu na nimefanikiwa kujiingizia kipato.

“Huwa nikitangaza vizuri mabao hasa ya klabu hizi kubwa Simba na Yanga mashabiki na hata waheshimiwa huwa wananipa kiasi cha fedha, sitaweka wazi ni kiasi gani, ila huwa naambulia chochote kitu.

“Mikoani huwa narudi na mchele, ndizi, Mwanza samaki na kadhalika. Achilia mbali vyakula, nimeshashonewa na mashati ya vitenge na mafundi, yote ni kutokana na utangazaji wangu ambao umekuwa ukiwafurahisha baadhi na kuwaumiza wengine na hii inatokana na ushabiki mkubwa uliopo kati ya Simba na Yanga hivyo siwezi kufurahisha pande zote kwa wakati mmoja lazima mmoja aumie,” anasema.

AMEWAPA UMAARUFU

Anasema kuwabatiza wachezaji majina hakuanza yeye, ilikuwapo tangu miaka ya nyuma, lakini na yeye amekuja kwa namna yake tofauti na walivyokuwa wanafanya watangazaji wa zamani kwa kuangalia namna ya uchezaji na kuwafananisha na nyota wengine.

“Zamani ilikuwa mchezaji kama anacheza kama fulani, mfano unamuangalia uchezaji wa Ibrahim Ajib unamlinganisha na staa kutoka nje ya nchi ndiyo unampachika jina, lakini mimi kwa upande wangu nimekuwa nikijaribu kuunganisha majina ya wachezaji wenyewe na huwa inaleta maana na kukubalika na wengi.

“Mfano MK14 nimechukua herufi za mwanzo za majina yake Meddie Kagere na namba yake ya jezi namba 14, jina ambalo limekuwa maarufu na limepokewa vyema na mchezaji mwenyewe.

Mwingine ni Heritier Makambo ambaye nakumbuka jina lake la utani nilimpachika katika mchezo wake wa kwanza wa ligi dhidi ya Mtibwa Sugar kwenye Uwanja wa Taifa, alifunga bao nikamwita Makambovic, jina ambalo limekuwa maarufu na kupokewa vizuri.”

“Jina hili lilitokana na fainali za Kombe la Dunia, mimi nilikuwa shabiki wa Croatia, timu yao ina nyota wengi ambao majina yao yanaendeana mfano Luka Modric na Ivan Rakitic hivyo baada ya nyota huyo wa Yanga kufunga bao hilo nikajikuta naunganisha jina na lilileta maana na kupokewa na mashabiki wengi ambao walitengeneza hadi jezi. Nyota mwingine ni Hassan Dilunga ‘HD’,” anasema.

ALIVYOKUTANA NA MAKAMBO, KAGERE

Kama unadhani kuna mchezaji amekasirika au hajapenda kuitwa majina aliyoyabuni Mpenja basi imekula kwako.

Unaambiwa baada ya nyota wa Yanga Makambo kusikia anaitwa Makambovic alipata kazi kumtafuta mtangazaji aliyempachika jina hilo kubwa akitaka kufahamu ni nani ili amshukuru.

“Unajua mara baada ya kutaja jina hilo lilikuwa maarufu sana na baadhi ya mashabiki waliprinti jezi zikiwa na jina hilo.

“Basi unaambiwa nilipigiwa sana simu na watu wa Yanga wakiniambia Makambo anataka kunifahamu, nikasema nikipata muda nitamtafuta. Basi kuna siku alikuja ofisini kwetu na kocha ndipo alipoonyeshwa kuwa mimi ndio nilimpa jina, alifurahi sana.

“Siyo Makambo tu hata MK14 alifanya hivyo, alinitafuta na kunishukuru. Aliniambia jina hilo limekuwa maarufu hadi kwao na kuweka wazi amekuwa akilitumia katika akaunti zake za mitandao ya kijamii kutokana na kuwa maarufu zaidi ya jina lake halisi, nafurahi kuona vitu ninavyofanya vinapokewa vizuri,” anasema.

USIMBA NA UYANGA UNAVYOMTESA

Unaambiwa pamoja na kutokuwa na mapenzi na timu yoyote ya Ligi Kuu Bara, Mpenja amekuwa akihusishwa katika ushabiki kitu ambacho kimekuwa kikimnyima raha na kumfanya aendelee kupambana zaidi kuwatoa watu katika mitazamo yao kwa kuwa sawa kila upande.

“Huwezi kuamini mimi sina mapenzi na timu yoyote inayoshiriki Ligi Kuu Bara.

“Kazi yangu ninayoifanya hainiruhusu kufanya hivyo, lakini bado nimekuwa nikiundiwa zengwe na mashabiki mimi ni mpenzi wa moja ya timu kati ya Simba na Yanga kutokana na utangazaji wangu.

“Sina na sijawahi kutangaza tofauti, kila mchezo ninaopewa kazi kuufanya, huwa nafanya kama inavyotakiwa, lakini nashangazwa na baadhi ya watu kunitengenezea matukio ambayo yananifanya niwe na wakati mgumu. Hiyo ni moja ya changamoto inayonipa shida katika kazi yangu,” anasema.

Unajua hapa Bongo

anamkubali nani zaidi?

Messi na Ronaldo je? Endelea naye tena kesho Alhamisi kufahamu mengi zaidi ya mtangazaji huyu anakuja juu kwa kasi.