Mourinho macho kodo kwa mastaa wa Croatia

Muktasari:

Mourinho anataka kujenga kikosi chake kwa kusajili mshambuliaji baada ya Manchester United kuanza Ligi Kuu kwa matokeo yasiyoridhisha na sasa ipo nafasi ya nane katika msimamo wa ligi

MANCHESTER, ENGLAND. Kocha wa Manchester United, Jose Mourinho yupo sokoni kusaka viungo wa ushambuliaji ambao wanakuwa na kasi wanapokuwa na mpira kwenye miguu yao ili kuifanya timu hiyo kuwa na makali ya kiwembe kwenye fowadi yake.

Kwenye mpango huo wa kunasa viungo wenye kasi ili kuifanya timu hiyo kuvusha mipira haraka kuelekea kwenye goli la wapinzani, Mreno huyo ameingia sokoni kuwasaka mastaa wawili wa Croatia, Ivan Perisicna Ante Rebic kuhakikisha wanatua Old Trafford.

Kuhusu mpango wa kuwanasa wachezaji hao hiyo imekuwa meseji ya wazi kabisa ambayo Mourinho alimwambia makamu mwenyekiti wa Man United, Ed Woodward, ambaye ndiye hasa anayehusika na masuala ya usajili.

Staa wa Inter Milan, Perisic na wa Eintracht Frankfurt, Rebic wote walikuwa kwenye rada za Mourinho katika dirisha lililopita la uhamisho wa majira ya kiangazi, lakini walishindwa kuwanasa baada ya kutajiwa bei iliyochangamka.

Inter Milan walihitaji Pauni 48 milioni na Man United hawakuwa tayari, Mourinho akigoma kulipa zaidi ya Pauni 45 milioni, huku mabosi wa klabu hiyo waligoma kulipa zaidi ya Pauni 40 milioni kwa mchezaji Rebic. Mourinho amezindua upya pia mpango wake wa kumnasa kiungo wa Lazio na timu ya taifa ya Serbia, Sergej Milinkovic-Savic.