Mourinho kalikoroga huko Spurs ni mshikemshike

Muktasari:

Spurs haijashinda mechi yoyote ya Ligi Kuu England kati ya nne zilizopita na walipata bao moja tu kwenye mechi tatu kabla ya mchezo wa usiku wa jana Jumatano walipotarajia kuwakabili Norwich City.

LONDON, ENGLAND. JOSE Mourinho yupo kwenye hatari ya kugomewa na wachezaji wake huko Tottenham Hotspur baada ya kudaiwa kuwafundisha mbinu zake za kizamani zinazokosa mvuto mazoezini.

Mastaa wakubwa kwenye kikosi hicho cha Spurs wanadai kwamba timu inaharibika chini ya Mourinho kutokana na mbinu zake za kutumia mipira mirefu kwamba ni kitu kinachowarudisha nyuma kwenye kumudu soka la kisasa.

Kuna wasiwasi pia kwamba staa aliyesajiliwa kwa pesa iliyovunja rekodi kwenye klabu hiyo, Tanguy Ndombele akapotea kabisa baada ya kocha huyo kusema hadharani kwamba kiungo huyo aliyenaswa kwa Pauni 65 milioni bado hayupo fiti kucheza England.

Spurs haijashinda mechi yoyote ya Ligi Kuu England kati ya nne zilizopita na walipata bao moja tu kwenye mechi tatu kabla ya mchezo wa usiku wa jana Jumatano walipotarajia kuwakabili Norwich City.

Taarifa zinadai kwamba wachezaji kadhaa wa kikosi cha kwanza cha Mourinho — ambao mwanzoni walimkaribisha kwa mikono yote Mreno huyo kutokana na kuwa na CV kubwa — wameripotiwa kuchoshwa na mbinu za Mreno huyo ikiwa ni miezi miwili tu tangu akabidhiwe timu.

Mazoezini kunadaiwa kuwekwa msisitizo wa kupiga mipira mirafu na kurusha mipira kama vile wapo kwenye ligi cha mchangani. Wachezaji wengi wa kikosi hicho wanasema kwamba wanarudishwa nyuma baada ya soka kubwa la ubunifu walilokuwa wakifundishwa na Mauricio Pochettino.

Jambo hilo linadaiwa kwamba linaweza kumweka pabana Mourinho, hasa kwa kipindi hiki ambacho hatakuwa na uhakika wa kuwa na pesa kusajili wachezaji watakaoendana na mfumo wake huku akipanga kumwondoa kabisa kikosini kiungo Christian Eriksen.