Mourinho atetea wachezaji Spurs

Muktasari:

Mourinho anaamini kama Spurs ingetangulia kupata bao kabla ya RB Leipzig mechi ingekuwa tofauti na wangeondoka na ushindi, lakini bahati mbaya kwao hilo halikutokea.

LONDON, ENGLAND . KOCHA wa Tottenham Hotspur, Jose Mourinho amewatetea wachezaji wake, licha ya kukubali kichapo cha bao 1-0 nyumbani kutoka kwa RB Leipzig katika mechi ya 16 bora ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.

Akizungumza baada ya mchezo huo, Mourinho alisema kuwa wachezaji wake walifanya kila waliloweza kupata matokeo kwenye mechi hiyo, lakini bahati mbaya kwao ni kuwa alikutana na timu bora yenye wachezaji waliokwenye kiwango cha juu kwa sasa.

“Tunatakiwa kuheshimu kilichofanywa na vijana na tuwaambie kuwa wamefanya kila walichoweza.” Alisema Mourinho. “Hivi unajua idadi ya siku ambazo Lamela (Erik) amefanya mazoezi ya timu?

“Sifuri, ametoka majeruhi na moja kwa moja kuingia kwenye timu na kucheza dakika 20 za mechi ya Ligi ya Mabingwa Ulaya. Hiyo ndiyo timu yetu. Ukiiangalia unaona vitu viwili, moja kundi la vijana safi sana wanaofanya kila kitu kuhakikisha wanashinda.

“Kitu cha pili unaona hali ilivyo kwa sasa. Ukiangalia wapinzani wako, wana Schick (Patrik), Werner (Timo) na Nkuku (Christopher). Nkuku akichoka anaingia Forsberg (Emil), Schick akichoka anaingia Poulsen (Yussuf), sisi hali yetu tete. Ni sawa na kwenda vitani na bunduki isiyokuwa na risasi.”

Mourinho anaamini kama Spurs ingetangulia kupata bao kabla ya RB Leipzig mechi ingekuwa tofauti na wangeondoka na ushindi, lakini bahati mbaya kwao hilo halikutokea.

Kocha huyo anaenda mbali zaidi kusema kwamba kuna wakati walikuwa na bahati kuendelea kubaki mchezoni kwa sababu kipa wao aliokoa michomo mwili muhimu ambayo kama ingejaa wavuni basi mechi ingeishia London.

Akizungumzia matokeo hayo kuelekea mechi ya marudiano, Mourinho alisema “Sihofii matokeo ya 1-0, kwa sababu kwa matokeo ya 1-0 mchezo bado uko wazi. Tunaweza kwenda pale na kushinda mechi na kusonga mbele.

‘Kinachonitisha ni kuwani ukweli kuwa tuna mechi nyingi zimefuatana na hatuna wachezaji wengi waliofiti. Tutamuona Lucas (Moura) akiwa amechoka kabisa, Bergwijn (Steven) pia na Lo Celso (Giovan), hili ni tatizo kwetu.”

Kocha huyo anaamini ugumu wa ratiba unaitesa zaidi klabu yake na kuiweka kwenye wakati mgumu k, japokuwa bado hajakata tamaa nafasi ya timu yake kuitoa RB Leipzig.