Mourinho atania apewe ubingwa wa Man City

Muktasari:

Huko England, Man City bado haijapewa adhabu yoyote huku ikiripotiwa Ligi Kuu England inapanga kufanya uchunguzi wa ndani kuona matumizi hayo ya pesa yalivyoipa faida kuliko timu nyingine.

LONDON, ENGLAND . JOSE Mourinho ametania Manchester United ilipaswa kubeba ubingwa wa Ligi Kuu England 2018 baada ya Manchester City waliokuwa mabingwa kugundulika kwamba, walicheza mchezo mchafu kwenye matumizi makubwa ya pesa katika usajili usioendana na kipato chao.

Jambo hilo limesababisha Man City kupigwa adhabu ya kutoshiriki kwa misimu miwili Ligi ya Mabingwa Ulaya na kupiga faini ya Pauni 25 milioni na Shirikisho la Soka la Ulaya, Uefa.

Huko England, Man City bado haijapewa adhabu yoyote huku ikiripotiwa Ligi Kuu England inapanga kufanya uchunguzi wa ndani kuona matumizi hayo ya pesa yalivyoipa faida kuliko timu nyingine.

Kama hilo litafanyika, basi Man City inaweza kunyang’anywa mataji manne kuanzia tangu iliposhinda 2012. Man City ilimaliza vinara kwenye ligi mwaka 2018, pointi 19 juu ya Man United iliyomaliza kwenye nafasi ya pili.

Mourinho, ambaye kwa sasa ni kocha wa Tottenham Hotspur wakati huo alikuwa Man United na amesema hivi:

“Nataka kuuliza kama timu iliyomaliza namba mbili mwaka 2018 itakuwa bingwa. Ndio au hapana? Hilo litavutia zaidi, lakini ni utani tu, mi nimeamua kutulizana tu. Hiyo ni adhabu waliyopewa na Uefa na bado wana nafasi ya kukata rufaa.”