Mourinho ampa tano Solskjaer

Muktasari:

Timu hizo zimekutana mara 194 na Man United ikishinda mara 92, Spurs 53 na sare 48.

MANCHESTER, ENGLAND. KOCHA wa Tottenham Hotspur, Jose Mourinho amesema licha ya kuifunga Manchester United mabao 6-1 jana katika mchezo wa Ligi Kuu, England kocha wa timu hiyo Ole Gunnar Solskjaer ameifanya timi hiyo iimarike.

Katika mchezo huo ambao ulichezwa katika dimba la Old Trafford Man United ilicheza pungufu kuanzia dakika ya 28, baada ya Antony Martial kutolewa nje kwa kadi nyekundu kwa kosa la kumpiga kiwiko Eric Lamela.

"Nikiangalia timu kwa sasa kuna mabadiliko makubwa, amebadilisha sehemu nyingi tofauti na ilivyokuwa hapo awali," alisema.

"Sikumbuki ni lini nilipoteza mechi kwa mabao 6, lakini nishawahi kufungwa 4 na 5, najua maumivu yake, nafahamu hatoweza kulala kwa amani, msinifikirie vibaya, kweli kwamba nahitaji kushinda tena zaidi ya mabao sita lakini mimi ni kocha nafahamu leo imemtokea yeye na kesho inaweza kuwa kwangu," aliongeza.

Baada ya matokeo hayo Spurs imepanda hadi nafasi ya sita ikiwa na alama saba, huku Man United ikishuka hadi nafasi ya 16, baada ya kukusanya alama tatu.

Hiyo inakuwa ni mara ya tatu kwa Man United kupoteza kwa idadi hiyo ya mabao baada ya kuwahi kukutana na aibu hiyo Oktoba, 1996 dhidi ya Southampton na 2011 kutoka kwa Manchester City.