Mourinho alipokabiliana na timu zake za zamani

Muktasari:

Jumamosi iliyopita kilipigwa kipute cha kuzikutanisha timu zinazowania nafasi hizo, Chelsea na Spurs. Mechi hiyo ilimrudisha kocha Jose Mourinho kwenda kucheza dhidi ya klabu yake ya zamani huko Stamford Bridge.

LONDON, ENGLAND. UHAI mpya umepatikana kwenye mbio za kufukuzia nafasi ya kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya huko kwenye Ligi Kuu England baada ya uamuzi wa Uefa kuamua kuifungia Manchester City kushiriki michuano hiyo kwa misimu miwili ijayo.

Hii ina maana, timu yoyote itakayomaliza msimu wa Ligi Kuu England msimu huu itakuwa na nafasi ya kucheza michuano hiyo ya Ulaya msimu ujao kama Man City watamaliza ndani ya Top Four, huku adhabu yake ikiendelea kubaki kama ilivyo.

Kwenye Ligi Kuu England, timu zinazochuana kuwania nafasi ya kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao ni pamoja na Chelsea, Tottenham Hotspur, Manchester United na Arsenal wakiwania nafasi hizo mbili, nne na tano ili kukamatia tiketi hiyo.

Chelsea wapo kwenye nafasi ya nne, Man United nafasi ya tano, wakati Spurs wapo kwenye namba sita na Arsenal kwenye nafasi ya tisa. Hapo katikati kuna Sheffield United kwenye nafasi ya saba na Wolves nafasi ya nane. Kwenye Top Three, zimejipanga Liverpool, Manchester City na Leicester City.

Jumamosi iliyopita kilipigwa kipute cha kuzikutanisha timu zinazowania nafasi hizo, Chelsea na Spurs. Mechi hiyo ilimrudisha kocha Jose Mourinho kwenda kucheza dhidi ya klabu yake ya zamani huko Stamford Bridge.

Wakati timu hizo mbili zilipokuwa zikiingia uwanjani zilitofautiana pointi moja tu, Chelsea 41 kwenye nafasi ya nne, Spurs 40 kwenye nafasi ya tano, lakini baada ya matokeo, Chelsea pointi 44 kwenye nafasi hiyo hiyo ya nne, Spurs wamebaki na pointi zao 40, lakini wameshuka hadi nafasi ya sita. Hicho ndicho kilichotokea.

Hii ina maana, Mourinho alikumbana na kichapo alipokwenda kukutana na timu yake ya zamani. Hata hivyo, hayo yalikuwa marudio tu, kwani kwenye mechi ya kwanza ambayo Mourinho alikutana na Chelsea akiwa nyumbani, kikosi chake cha Spurs kilichapwa 2-0, Desemba mwaka jana.

Kwenye mechi hiyo ya marudiano huko Stamford Bridge, Mourinho na timu yake walichapwa tena, safari hii mabao 2-1, Frank Lampard akimwonyesha ubabe kocha wake wa zamani mar azote mbili.

Mourinho alimnoa Lampard wakati alipokuwa kwenye kikosi cha Chelsea, lakini baada ya kurudi kwenye Ligi Kuu England kuchukua mikoba ya kuinoa Spurs, amekabiliana na mchezaji wake huyo wa zamani akiwa kocha huko Stamford Bridge.

Nje ndani, Mourinho ametulizwa na Lampard na kumfanya aweke rekodi mbovu dhidi ya timu zake za zamani tangu alipojiunga na Spurs.

Mwanaspoti linakutelea mara zote ambazo Mourinho alikumbana na timu zake za zamani na matokeo yake aliyovuna.

Mourinho vs Benfica – mechi 4, ushindi 3

Kocha Mourinho muda wake aliokuwa Benfica ulikuwa mfupi sana, lakini bado ameingia kwenye rekodi tamu katika klabu hiyo. Aliongoza timu hiyo katika mechi 11 na mpango wa kupewa mkataba mpya katikati ya msimu wa 2000/01 ulikataliwa na rais wa timu, Manuel Vilarinho na hivyo kumfanya Mourinho ajiuzulu kuinoa timu hiyo haraka.

Baadaye, Vilarinho alikiri kufanya makosa kwa kushindwa kumpa mkataba mpya Mourinho. Baadaye, Mourinho akanaswa na Uniao De Leiria, mahali ambako alienda kuonyesha ubora mkubwa na kuivutia FC Porto kumpa kazi.

Kwa muda wake aliokuwa kwenye klabu hiyo, Mourinho hakupoteza, alishinda dhidi ya Benfica na kutoa sare tu. Aliwachapa tena Benfica alipokuwa na Man United alipokutana nao kwenye makundi ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.

Mourinho vs Uniao De Leiria – mechi 3, ushindi 3

Mourinho alifurahia mafanikio makubwa kwenye FC Porto, akishinda Primeira Liga mara mbili, Taca de Portugal mara moja, Kombe la UEFA na Ligi ya Mabingwa Ulaya na lilikuwa taji la kwanza la Ulaya kwa Porto tangu mwaka 1987. Mechi yake ya kwanza dhidi ya timu yake ya zamani kwenye kombe la Taca de Portugal, Agosti 2003, FC Porto walishinda 1-0.

Mourinho amecheza dhidi ya Uniao mara tatu na kushinda zote, huku timu yake ikifunga mabao sita na kufungwa mawili tu. Matokeo mengine aliifunga timu hiyo 3-1 ugenini na 2-1 nyumbani, hivyo akiwa na ushindi asilimia 100 kwenye mechi alizocheza na timu yake ya zamani ya Uniao De Leiria.

Mourinho vs FC Porto – mechi 6, ushindi 3

Mourinho alibeba mataji ya kutosha akiwa na FC Porto huko Ureno na hilo lilitosha kuwavutia Chelsea kwenda kunasa huduma yake.

Mourinho aliinoa Chelsea kwenye awamu mbili, awamu yake ya kwanza, alikabiliana na timu yake ya zamani ya FC Porto mara nne, alipoteza mara moja tu katika mechi hizo, ugenini kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya, Desemba 2004. Hata hivyo, mechi hiyo haikuwa na umuhimu sana kwa Mourinho kwa sababu, Chelsea tayari ilikuwa imeongoza kundi lake.

Katika awamu yake ya pili kwenye kikosi cha Chelsea, Mourinho alishinda mara moja dhidi ya Porto na kupoteza nyingine na kipindi hicho Porto ilikuwa chini ya Mhispaniola Julen Lopetegui. Mechi sita za Mourinho dhidi ya Porto, ameshinda tatu, sare moja na vichapo viwili, huku akifunga mabao 10 na kufungwa saba.

Mourinho vs Real Madrid – mechi 1, ushindi 0

Mourinho baada ya kuachana na Real Madrid alipata nafasi ya kuchuana na timu yake hiyo ya zamani. Hii ilikuwa wakati alipokuwa kwenye kikosi cha Man United na alikwenda kuwakabili Los Blancos katika mchezo wa Uefa Super Cup. Katika mechi hiyo iliyopigwa Agosti 8, 2017, ambapo Man United walikuwa mabingwa wa Europa League na Real Madrid mabingwa wa Ligi ya Mabingwa Ulaya, hivyo mabingwa wa makombe ya Ulaya walikutana kufungua msimu mpya. Mechi hiyo ilimalizika kwa Real Madrid kuichapa timu ya Mourinho mabao 2-1. Mechi moja ya Mourinho aliyocheza dhidi ya Real Madrid imeishia kwa kuchapwa, huku timu yake ikifunga bao moja na kufungwa mabao mawili.

Mourinho vs Chelsea – mechi 11,

ushindi 4

Kumekuwa na hisia nyingi tofauti inapokuja suala la Mourinho kukumbana na Chelsea, timu inayodaiwa aliinoa kwa mapenzi yake yote. Awamu zake mbili alizokuwa kwenye timu hiyo na kuondoka, Mourinho amekabiliana na Chelsea mara kibao, akiwa na Man United na baadaye akiwa Spurs.

Lakini, alikabiliana na Chelsea pia hata alipokuwa akiinoa Inter Milan. Kwa jumla yake, amekutana na Chelsea mara 11, huku mara nne tu ndio alishinda, akitoka sare moja na kuchapwa mara sita. Ushindi wake wa kwanza dhidi ya Chelsea ulikuwa akiwa Inter Milan na alishinda mara zote mbili kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya hatua ya robo fainali msimu wa 2009/10.

Lakini, alipokwenda Man United, mechi yake ya kwanza aliyorudi Stamford Bridge alichapwa 4-0 kwenye ligi, kisha akafungwa tena 1-0 kwenye Kombe la FA. Chelsea imeonekana kumtesa zaidi Mourinho, akiteswa tangu akiwa na Man United na sasa Spurs na kwenye mechi mbili alizokabiliana na The Blues, amechapwa zote. Timu yake Mourinho dhidi ya Chelsea imefunga mabao 10, wakati yenyewe imefungwa 15.

Mourinho vs Man United – mechi 1, ushindi 0

Mourinho amepoteza mechi yake ya kwanza aliyocheza dhidi ya timu yake ya zamani, Manchester United. Hii imetokea baada ya sasa kuinoa Spurs, ambapo kwenye mchezo wa Ligi Kuu England alipowakabili wababe hao wa Stamford Bridge alikumbana na kichapo cha mabao 2-1, Marcus Rashford akifunga yote hayo mawili, huku Mourinho na Spurs yake bao lao la kujifariji lilifungwa na Dele Alli.

Hiyo ina maana katika mechi hiyo moja aliyowakabili Man United, Mourinho timu yake imefunga bao moja na kuchapwa mawili, huku ikiwano na wastani wa ushindi wa asilimia sifuri.

Huko kwenye kikosi cha Spurs, Mourinho ni kama amekuwa na mikosi kutokana na wachezaji kibao muhimu kwenye kikosi chake kuwa majeruhi wakiwamo washambuliaji muhimu, Harry Kane na Son Heung-min.

Rekodi za jumla

za Mourinho

Kwenye rekodi za jumla za Mourinho alicheza dhidi ya timu zake za zamani, kocha huyo amefanya hivyo kwenye mechi 26, akishinda 13, sare tatu na vichapo 10. Mourinho ameshinda mabao 35 na kufungwa 28, huku akiwa na wastani wa ushindi wa asilimia 52.