Mourinho aibuka, aiponda Manchester United

Muktasari:

  • Mourinho pia anaamini kwamba wachezaji wa zama hizi wamekuwa laini sana akatolea mfano wa mchezaji mmoja ambaye alimwambia kwamba asimkosoe mbele ya wenzake.

LONDON, ENGLAND.BADO Jose Mourinho ana kitu moyoni. Hajamalizana na Manchester United. Ana hasira nao. Safari hii ameibuka ghafla na kuvunja ukimya huku akiwalaumu waajiri wake wa zamani kwamba hawakumpa sapoti ya kutengeneza timu imara.

Mourinho amefungua kifua chake na kuweka wazi kwamba anaamini makocha wenzake, pep Guardiola wa Manchester City na Jurgen Klopp wa Liverpool waliandaliwa mazingira ya kuwania ubingwa na matajiri wao.

Mourinho aliyefukuzwa Desemba mwaka jana baada ya mwenendo mbovu wa United katika Ligi Kuu anaamini kwamba wenzake walipewa pesa za kutosha kujenga vikosi vyao lakini yeye hakupewa pesa ya kutosha na ndio maana ilikuwa ngumu kwake kupata mafanikio “Chukulia mfano wa Manchester City, katika msimu wake wa kwanza Guardiola hakuchukua ubingwa. Mambo yalikuwa magumu na watu walikuwa wanatazamia Manchester City itwae kombe. Walikuwa wamekuja kutoka katika vipindi vya ushindi. Walikuwa mabingwa chini ya (Roberto) Mancini na (Manuel) Pellegrini. Baadhi ya wachezaji tayari walikuwa mabingwa mara mbili, (Sergio) Aguero na (Vincent) Kompany, katika msimu wa pili Pep alichukua maamuzi makubwa, lakini. Matumuzi yake makubwa yalipewa sapoti.”

“Kwa mfano, hakuwataka (Pablo) Zabaleta au (Bacary) Sagna, walinzi wawili wa pembeni hao, lakini pia hakuwataka (Aleksander) Kolarov au (Gael) Clichy. Katika dirisha kubwa aliuza mabeki wake wote wa pembeni na akawapata (Kyle) Walker, Danilo, (Benjamin) Mendy na mwingine. Alipewa sapoti.” Aliongeza Mourinho.

“Pale Liverpool najiuliza wachezaji wangapi walikuwepo kabla ya Jurgen kuwasili? Hakuwepo Alisson (Becker), hakuwepo (Virgil) Van Dijk, hakuwepo (Andrew) Robertson, hakuwepo (Mohamed) Salah, hakuwepo (Roberto) Firmino, hakuwepo (Sadio) Mane, hakuwepo Fabinho, hakuwepo (Georginio) Wijnaldum, hakuwepo (Naby) Keita” alisema Mourinho.

“Ninapozungumzia kuhusu uongozi, kuhusu muundo wa klabu, sio suala la uongozi tu, ni kila kitu, hata katika mawazo ya soka. Wewe kama ni kocha na una mkono katika kuchagua wachezaji unaowataka ambao watafuata falsafa zako za soka, au kufuata njia fulani ya kucheza katika michuano fulani. Wakati mwingine unashindwa kufanya hivyo.” Aliongeza Mourinho akimaanisha jinsi alivyoshindwa kuwapata wachezaji sahihi.

Mourinho pia anaamini kwamba wachezaji wa zama hizi wamekuwa laini sana akatolea mfano wa mchezaji mmoja ambaye alimwambia kwamba asimkosoe mbele ya wenzake.

“Nilikuwa na mmoja kati ya wachezaji wangu namfundisha, na ninapofundisha napenda kuwa huru na najiona kama niko katika familia na nipo huru kumkosoa mtu yeyote. Kuna mchezaji mmoja aliwahi kuniambia kwa upole ‘tafadhali unaponikosoa unaweza kufanya hivyo tukiwa wawili tu? nikamuuliza kwanini akajibu ‘Kwa sababu kwa jinsi nilivyo ukinikosoa mbele ya wachezaji wengine sijisikii vema. Alikuwa mmoja kati ya wachezaji bora wa kizazi chake. Siku hizi inabidi uwe makini kuwaelewa wachezaji na tabia zao.”

Mourinho amedai kwamba atarudi kibaruani haraka iwezekanavyo huku akidai kwamba tayari amekataa ofa za klabu tatu tangu alipofukuzwa na manchester United.