Mourinho aendelea kumchimba Paul Pogba

Muktasari:

  • Mourinho ameelezea jinsi ambavyo tukio la staa huyo kugomea kupanda basi la timu lilivyotokea wakati walipokwenda kucheza na Burnley na kushinda mabao 2-0 siku chache kabla ya Pogba kuvuliwa kitambaa cha unahodha msaidizi Septemba mwaka jana.

LISBON,URENO.BADO kuna kitu kimekaa katika kifua cha kocha wa zamani wa Manchester United, Jose Mourinho. Ana dukuduku lake moyoni. Safari hii amemshukia mchezaji anayetajwa kuwa ni Paul Pogba katika semina ya makocha aliyoendesha kwao Ureno.

Mourinho ameelezea jinsi alivyoyumbishwa na mchezaji mmoja mwenye maringo katika utawala wake pale Old Trafford na ingawa hakutaja jina lakini imeelezwa alikuwa anamzungumzia staa huyo wa kimataifa wa Ufaransa.

Kocha huyo Mreno alimvua unahodha Pogba mwanzoni mwa msimu huu huku akitajwa kuwa na migogoro mingi na staa huyo lakini katika mahojiano haya anaelezea jinsi ambavyo staa huyo kuna wakati alitaka kupanda gari lake binafsi baada ya mechi na si basi la timu. Akaelezea jinsi ambavyo angeweza kufukuzwa kwa kukosea kumlea mchezaji huyo.

Mourinho ameelezea jinsi ambavyo tukio la staa huyo kugomea kupanda basi la timu lilivyotokea wakati walipokwenda kucheza na Burnley na kushinda mabao 2-0 siku chache kabla ya Pogba kuvuliwa kitambaa cha unahodha msaidizi Septemba mwaka jana.

“Tulicheza na timu ambayo ilikuwa kilomita 30 tu kutoka Manchester na kuna mchezaji aliniuliza kama angeweza kurudi Manchester kwa kutumia usafiri wake binafsi,” alianza Mourinho wakati akiwa katika semina ya ukocha kwao Ureno.

“Nikamwambia ‘Kama tungekwenda London na ungetaka kubakia pale, hicho kingekuwa kitu kinachowezekana. Lakini hapa ni karibu, haileti maana yoyote ile’, jamaa alikasirika. Halafu tukashinda ile mechi na akaniomba tena. Kwa sababu nilikuwa na furaha nikaamua kumpa sharti dogo tu ‘Basi panda basi halafu mwambie dereva wako akichukue dakika 10 tu baada ya kuondoka uwanjani kisha nenda unapotaka’. Bado huyu jamaa hakuwa na furaha. Nilikwenda katika mkutano na waandishi wa habari na nilipokwenda katika basi la timu nililikuta gari lake Rolls-Royce limepaki likiwa na dereva wake,” anasema Mourinho.

“Gari lake lilikuwa jipya na ‘Mheshimiwa’ angependa kuondoka uwanjani na Rolls-Royce lake. Sasa unashughulika vipi na jambo hili? Unamwambia aondoke na gari lake? Nimwambie aende wakati nina furaha? Au unashughulika na suala hilo kwa njia zako na unafukuzwa kazi?” Alihoji Mourinho.

Pogba kwa sasa amekuwa katika kiwango kizuri chini ya kocha mpya, Ole Gunnar Solskjaer licha ya United kuendelea kusuasua katika msimamo wa Ligi ya England ambapo juzi Jumanne ilichapwa mabao 2-1 ugenini kwa Wolves na kuiacha timu yao ikiwa njia panda kwenda katika michuano ya Ligi ya Mabingwa.

Kichapo cha juzi kimeiacha ikiwa katika nafasi ya tano ikiwa na pointi 61 na endapo Chelsea ingeshinda pambano la jana Jumatano dhidi ya Brighton United ilitazamiwa kushuka hadi nafasi ya sita katika msimamo wa Ligi Kuu. Nafasi itakayobaki kwa United kucheza Ligi ya Mabingwa msimu ujao itategemea kama itafanikiwa kuchukua ubingwa wa Ulaya msimu huu huku wiki ijayo wakitazamiwa kucheza pambano kali la Ligi ya Mabingwa dhidi ya Barcelona.

Katika pambano lijalo la Ligi United ambayo United inayumba katika safu yake ya ulinzi itamkosa beki wake wa kulia na nahodha wa timu kwa sasa, Ashley Young ambaye alionyeshwa kadi nyekundu na mwamuzi Mike Dean. Mwamuzi huyo sasa amewekwa rekodi ya kuwa mwamuzi wa kwanza kuonyesha kadi nyekundu tatu.

Young atalikosa pambano dhidi ya West Ham huku United ikikabiliwa na ratiba ngumu katika ligi ambapo baada ya hapo itacheza ugenini dhidi ya Everton kabla ya kurudi nyumbani kukipiga na Manchester City.