Mourinho anukia Asernal kimyakimya

Muktasari:

April mwaka huu, Mourinho pia alikataa kazi ya ukocha katika klabu tajiri ya Guangzhou Evergrande ya China ambayo ilimpa mkataba wa Euro 100 milioni ambao ungemfanya kuwa kocha anayewahi kulipwa pesa nyingi zaidi katika historia ya soka duniani.

LONDON, ENGLAND . KAMA unaweza kujumlisha mambo basi hesabu zinaweza kuwa rahisi. Kocha wa zamani wa Chelsea na Manchester United, Jose Mourinho amewaambia rafiki zake anataka kuwa kocha wa kwanza England kuchukua ubingwa wa England na Ulaya na klabu tofauti.

Hilo linaweza kuinufaisha Arsenal ambayo imetabiriwa inaweza kuanza mchakato wa kutafuta kocha mpya muda si mrefu kuanzia sasa kama kocha wao, Unai Emery ataendelea na mwendo wa kusuasua klabuni hapo.

Mourinho amekuwa hana kazi tangu alipotimuliwa na Manchester United Desemba mwaka jana baada ya matokeo mabovu pamoja na mahusiano yake mabovu na wachezaji na nafasi yake ilichukuliwa na kocha wa sasa, Ole Gunnar Solskjaer.

Kuanzia hapo amegomea kazi nyingi zilizoletwa mezani kwake na inadaiwa klabu za Sporting Lisbon, Borussia Dortmund na Lyon ya Ufaransa ziliweka ofa mezani kwake lakini akaona hazina hadhi ya kwenda kufundisha.

April mwaka huu, Mourinho pia alikataa kazi ya ukocha katika klabu tajiri ya Guangzhou Evergrande ya China ambayo ilimpa mkataba wa Euro 100 milioni ambao ungemfanya kuwa kocha anayewahi kulipwa pesa nyingi zaidi katika historia ya soka duniani.

Inaaminika kwamba lengo la Mourinho ni kuendelea kubakia katika Ligi Kuu ya England na kuacha rekodi isiyofutika kwa urahisi huku mpaka sasa kukiwa hakuna kocha ambaye amewahi kutwaa mataji matatu ya Ligi au Ulaya akiwa na klabu tatu tofauti.

Kama Mourinho akifanya hivi ataheshimika zaidi katika soka.

Huku kocha wa Spurs, Mauricio Pochettino akiwa anatazamwa zaidi na Manchester United na Real Madrid, Tottenham inajua kwamba wanaweza kumfukuzia Mourinho endapo wataachana na kocha wao Muargentina.

Lakini wakati huu Unai Emery akianza kuwa katika presha kubwa Arsenal, Washika Bunduki hao wanaweza kujikuta wakisaka kocha mpya na Mourinho ameiweka Arsenal katika ngazi ya juu miongoni mwa klabu anazoweza kufundisha.

Kocha huyo alikuwa uwanjani wakati Arsenal wakiichapa Vitoria Guimaraes ya kwao Ureno katika pambano la michuano ya Europa na alikuwa amealikwa na mmoja kati ya mabosi wa Arsenal katika masuala ya utawala wa soka klabuni, Raul Sanllehi.

Inaeleweka kwamba kuna majina ambayo yamekuwa yakihusishwa na kazi ya Unai Emery kama akifukuzwa ambapo makocha kama Mikel Arteta, Patrick Vieira, Brendan Rodgers wamekuwa wakihusishwa na kibarua hicho lakini jina la Mourinho kuna uwezekano mkubwa likajitokeza wakati huu akiwa hana kazi huku rekodi yake ikiwa kubwa zaidi kuliko wengine.

Emery anashutumiwa kuiacha Arsenal ikiwa katika mapungufu yale yale ambayo klabu hiyo ilikuwa nayo katika miaka ya mwisho ya kocha aliyepita, Arsene Wenger na mashabiki wameanza kumtolea kucha zaidi baada ya timu yao kuchapwa 1-0 ugenini na Sheffield United huku wakitoka sare ya 2-2 na Crystal Palace nyumbani licha ya kuongoza kwa mabao 2-0.

Kocha huyo pia amekuwa akishutumiwa na mashabiki wa Arsenal kwa kumtupa nje ya kikosi kiungo mahiri mchezeshaji wa timu hiyo, Mesut Ozil huku akiwapanga wachezaji wasio na uzoefu pamoja na kumpa kitambaa cha unahodha, Granit Xhaka.

Mourinho alitwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya England mara tatu na Chelsea huku pia akitwaa ubingwa wa Europa na United na anaamini anaweza kutwaa mataji hayo na timu nyingi ya tatu tofauti katika soka la England.

Familia ya Mourinho bado inaishi katika Jiji la London na ingawa pia amekuwa akihusishwa kuchukua kibarua cha Zinedine Zidane kama akifukuzwa kazi Real Madrid, lakini kazi ya Arsenal inaweza kumpa nguvu zaidi kwa vile bado hajawahi kufundisha timu hiyo tofauti na Real Madrid ambayo aliacha mpasuko nyuma yake.

Hivi karibuni baadhi ya mashabiki wa Arsenal mitandaoni walitaka kocha huyo apewe timu yao baada ya kuchambua vyema jinsi ambavyo staa mpya wa klabu hiyo, Nicolas Pepe aliyenunuliwa kutoka Lille kwa dau la Pauni 72 milioni anavyoweza kutumika kwa ajili ya kuonyesha makali yake.

Hata hivyo baadhi ya mashabiki walipinga Mourinho kupewa kibarua hicho kutokana na tabia yake ya kukorofishana wachezaji wake wa kikosi cha kwanza hasa wale mastaa kama alivyokorofishana na Paul pogba akiwa na Manchester United.