Mourinho, Southgate watibuana

 London, England. Gareth Southgate amemjibu kocha Jose Mourinho akimwambia: “Ni jukumu lako kujua maendeleo ya Harry Kane kwa ajili ya timu ya taifa ya England.

Kocha huyo wa Spurs, Mourinho alimtaka kocha wa ‘Three Lions’, Southgate kumheshimu Kane na kumpangia mechi za kumpa mapumziko kwenye mechi tatu zijazo za England katika Uwanja wa Wembley.

Lakini Southgate, ambaye anaangalia mafanikio ya mashindano ya Euro mwakani, alisema: “Kitu ambacho Jose anatakiwa kufanya ni kuhakikisha kuwa Aprili na Mei awe makini na Harry kwa ajili yetu, kwasababu kuna watu 55 milioni wanamtazama. Bila shaka, hiyo ni kazi ya pande mbili.

“Jose alikuwa katika kiwango kizuri, nilimsikia. Huwa hapigi simu, lakini atasimamajuu ya Uwanja wa Tottenham na kutuambia.

“Siwezi kuthibitisha kwamba mchezaji atacheza kwa dakika kadhaa katika mechi zote tatu, lakini tunathamini hali zao.

“Kwasasa hatuna mpango wa kuanzisha wachezaji wale wale katika mechi zote tatu. Lengo letu ni kukipa nafasi kikosi. Tunatakiwa kuwajibika. Msimu una changamoto nyingi.”

Southgate alitaja majina ya wachezaji 30 juzi kwa ajili ya mchezo wa kimataifa wa kirafiki dhidi ya Wales na mechi mbili za fainali za Kombe la Mataifa ya Ulaya dhidi ya Ubelgiji na Denmark.