Morrison kidedea, Yanga chalii

Muktasari:

Winga Morrison raia wa Ghana aliingia kwenye mvutano na Yanga ambayo ilidai imemuongezea mkataba wa miaka miwili baada ya ule wa miezi sita kumalizika na yeye kukataa kuwa hajasaini.

Sakata la Bernard Morrison na klabu ya Yanga limekwisha kwa mchezaji huyo kushinda, ingawa amepelekwa kamati ya maadili ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).

Mwenyekiti wa Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji ya TFF, Elias Mwanjala jioni hii Agosti 12, 2020 amesema mkataba wa Morrison na Yanga umeonekana na mapungufu.

"Kikao kilikuwa kirefu mpaka kufikia maamuzi haya, malalamiko ya Morrison yalikuwa kwamba hakuongeza mkataba na Yanga, tumeangalia mkataba wake tumeona una walakini  tumeona Yanga mkataba wao una utata kidogo,"

Aliongeza pia kuna mapungufu kwenye sehemu ya kusaini, imekatwa halafu hakuna sehemu ya waliosaini wote na kusema sheria inasema ukikata sehemu katika makaratasi basi inabidi umuite mwenzako asaini tena.

Mwanjala alisema wamempa Morrison nafasi ya kuchagua timu anayohitaji kucheza hata kama ni kurudi Yanga, ingawa imempeleka kamati ya maadili kwa kuingia mkataba mwingine wakati kesi yake na Yanga ikiwa inaendelea.

"Alikiri ameingia mkataba na Simba Agosti 8, hivyo kwa kosa hilo tumempeleka kamati ya maadili," amesema.

Akizungumzia mkataba na Yanga ambayo ilidai ni mchezaji wao hadi 2022, Mwanjala amesema unaonekana amesaini Machi 20 na mwingine Julai 15, hivyo mkataba huo ulikuwa na mapungufu, lakini kama Yanga ikihitaji kukata rufaa kama haijaridhika inaweza kwenda CAS