Morrison chini ya ulinzi mkali Chamazi

Muktasari:

Morrison alijiunga na Simba katika dirisha kubwa la usajili mwaka huu ambapo hadi sasa ameifungia mabao mawili huku akizalisha mengine manne katika mechi zote alizoichezea.

Licha ya Simba kushinda kwa mabao 3-1 dhidi ya Mlandege, winga Bernard Morrison amekuwa akichungwa vilivyo na walinzi wa Mlandege.

 

Mchezaji huyo aliyesajiliwa na Simba akitokea Yanga ndiye amekuwa akitazamwa zaidi na mabeki wa Mlandege ambao wamekuwa hawapungui wawili kumfuata kila anaposhika mpira.

 

Lakini haitoshi tu katika kumchunga bali pia mabeki hao wamekuwa wakimchezea rafu za mara kwa mara katika kile kinachoonekana ni mbinu ya kumpunguza kasi.

 

Rafu hizo zimepelekea mwamuzi Hery Sasii kupuliza filimbi za mara kwa mara na kuizawadia Simba, adhabu ndogo ambazo hata hivyo nyingi wameshindwa kuzitumia.

 

Ukiondoa Morrison, wachezaji wengine ambao wamekuwa wakifanyiwa faulo za mara kwa mara ni Luis Miquissone na Larry Bwalya.

 

Simba ilitawala mchezo na kucheza kana kwamba ipo mazoezini kwani muda mwingi imekuwa ikimiliki mpira, kutengeneza nafasi na kulishambulia lango la Mlandege mara kwa mara.

 

Pengine Simba ingekuwa imeshafunga idadi kubwa ya mabao lakini uhodari wa kipa wa Mlandege, Mohamed Abdallah kuokoa mashambulizi yao umewanyima fursa hiyo.

 

Moja ya mashambulizi hayo ni lile la dakika ya 68 ambapo kipa Abdallah aliokoa kwa ustadi krosi ya Ibrahim Ajibu ambayo Chris Mugalu alikuwa anajiandaa kuimalizia kwa kichwa.