Morrison aomba radhi Simba

MSHAMBULIAJI wa Simba, Bernard Morrison ameomba msamaha kupitia akaunti yake ya mtandao wa kijamii wa Instagram baada ya kufungiwa mechi tatu na faini ya Sh 500,000 kwa kosa la kumpiga ngumi beki wa Ruvu Shooting, Juma Nyoso.

Morrison alifanya madhambi hayo katika mechi ya Simba dhidi ya Ruvu Shooting iliyochezwa kwenye Uwanja wa Uhuru na adhabu hiyo ilitolewa na Kamati ya Uendeshaji na Usimamizi wa Bodi ya Ligi Kuu Bara (TPLB).

Kupitia mtandao huo wa kijamii Morrison aliandika "Samahani sana kwa matendo yangu kwenye mchezo uliopita,"

"Naomba msamaha kwani wote tunakifanya vitu kwa mapenzi ya klabu zifanye vizuri lakini wakati mwingine tunakosea.

"Nipo pamoja kiroho na nyie mashabiki na timu yetu Simba kwa mechi zote tatu," ameandika Morrison.

Tukio hilo lilitokea baada ya mpira kusimama dakika ya 72, kutokana na wachezaji wa timu zote mbili kuwa kwenye mzozo uliotokana na mwamuzi kuamua Simba ipige penalti baada ya mchezaji, Luis Miquissone kuonekana akichezewa faulo ndani ya boksi.

Adhabu hiyo itamfanya Morrison kukosa michezo mitatu ambayo dhidi ya Mwadui, Kagera Sugar na Yanga ambao umepangwa kupigwa Novemba 7, katika Uwanja wa Benjamini Mkapa.