Morrison amtikisa Z Anto

Muktasari:

Wapo baadhi ya mashabiki wa Yanga ambao wanaonekana kuumizwa endapo Benard Morrison atacheza Simba msimu ujao, miongoni mwao ni mwanamuziki wa kizazi kipya, Z Anto, aliyekiri kupenda uchezaji wa staa huyo.

MSANII wa Bongo Fleva, Z Anto amesema haamini kama kweli Benard Morrison atacheza Simba msimu ujao wa Ligi Kuu Bara na kukiri kwamba ikiwa hivyo itamuumiza.

Z Anto ameiambia Mwanaspoti Online leo Jumatatu Agosti 10, 2020 kuwa licha ya kumuona ni mchezaji huyo nidhamu yake ni ndogo, uwezo wake wa kuisaidia timu upo juu.

Z Anto ni shabiki wa Yanga kindakindaki, amesema kwa uwezo alionao Morrison alijipa moyo kwamba viongozi wangekaa naye chini kumjenga ili huduma yake iendelee kuwa na manufaa kwa timu.

Amesema Yanga imekosa mchezaji wa maana ambaye muda wote anakuwa msumbufu kwa timu pinzani.

"Niwe muwazi baada ya kuona Simba wameweka picha kwenye kurasa zake za mitandao ya kijamii wa Instagramu ilinishitua sana, nikachukulia kama ni uongo wa kutaka mashabiki wa Yanga tuumie,"

Ameongeza kuwa "Baada ya kuona mambo yanazidi kuwa magumu baina ya Simba na Yanga, ndio naanza kuamini kwamba inawezekana Morrison akawa amesaini Msimbazi, aisee itaniuma kiukweli kwani ni mchezaji mzuri ambaye ana uwezo wa kusaidia timu kwa kiasi kikubwa,"

Z Anto ambaye amewahi kutamba na kibao cha Binti Kiziwi amesema Yanga inahitaji wachezaji wenye uwezo wa kusumbua timu pinzani ndani ya dakika 90, hivyo usajili unaoendelea ameshauri viongozi wapate nyota watakaowatengenezea burudani msimu ujao.

"Ingawa kama Morrisn atacheza Simba nitachukulia ndio mpira kwani soka kwa mchezaji ni biashara, kikubwa tujipange namna ambavyo tutatafuta furaha ambayo tumeikosa ndani ya misimu mitatu mfululizo,"amesema.