Morrison aikosa Yanga kwa adhabu

Dar es Salaam. Kamati ya Saa 72 iliyo chini ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) imemfungia mwamuzi Shomary Lawi kutojihusisha na soka kwa muda wa mwaka mmoja baada ya kushindwa kumudu mechi kati ya Prisons na Simba iliyochezwa Uwanja wa Nelson Mandela, mjini Sumbawanga.

Wakati Lawi akikumbana na adhabu hiyo wachezaji watatu, Bernard Morrison (Simba), Juma Nyosso (Ruvu Shooting) na Salum Kimenya (Prisons) wao wamefungiwa mechi tatu.

Kwa maana hiyo, Morrison ataikosa mechi ya watani wa jadi Yanga inayotarajiwa kuchezwa Novemba 7, 2020, huku akianza kutumikia adhabu hiyo mechi ijayo dhidi ya Mwadui FC itakayochezwa Jumamosi jijini Dar es Salaam.

Nyosso naye ataanza kutumikia adhabu yake mechi ijayo ambapo timu yake itakutana na Coastal Union huku Kimenya ataanza kukaa nje kuanzia mechi dhidi ya Polisi Tanzania.

Nyosso amepewa adhabu hiyo baada ya kumwangusha Morrison katika mechi yao iliyopita ambapo Ruvu walishinda bao 1-0 huku Morrison ameadhibiwa kwa kumpiga Nyosso.

Kimenya amepewa adhabu hiyo kwa kosa la kumpiga Morrison kwenye mechi ambayo Prisons ilishinda bao 1-0.

Akizungumza Dar es Salaam jana, Mwenyekiti wa Kamati ya Saa 72, Steven Mnguto alikiri kamati yake kukutana na kutoa uamuzi huo kwa watajwa.

“Ni kweli tumekutana jana Jumanne (juzi) na kufanya uamuzi ambao utatangazwa baadaye baada ya kujiridhisha matukio tuliyoyapitia yaliyowahusu wahusika.

Kutokana na Mnguto, Morrison alihusika katika vurugu zilizotokea kwenye mchezo wa Simba dhidi ya Ruvu Shooting uliofanyika kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.

Katika mchezo huo, vurugu ziliibuka wakati Simba walipopata penalti kipindi cha pili na wachezaji wa Ruvu Shooting wakibishana na mwamuzi juu ya tukio lililosababisha adhabu hiyo.

Katika marudio ya picha za video, mshambuliaji huyo wa Simba alionekana akimpiga ngumi Juma Nyosso wa Ruvu Shooting na kukimbia kabla ya beki huyo wa zamani wa Simba na Kagera Sugar kuamka na kutaka kumrudishia.

Morrison hakupewa adhabu yoyote na mwamuzi kutokana na kushindwa kuliona tukio hilo.

Kwa upande wa Lawi, mchezo aliochezesha kati ya Simba na Tanzania Prisons unadaiwa kuwa chanzo kutokana na baadhi ya matukio kushindwa kuyaamua ipasavyo, ikiwamo la kuangushwa kwa Morrison.