Morrison, Yanga watinga polisi

Muktasari:

Mwenyekiti wa Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji ya TFF, Elias Mwanjala ndiye aliyefichua taarifa hizo katika mahojiano na Mwanaspoti.

LILE sakata la Bernard Morrison na klabu ya Yanga limefikia patamu baada ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kusema kuwa suala la kiungo mshambuliaji huyo kwa sasa linashughulikiwa na vyombo vya dola na litatolewa amuzi mwanzoni mwa mwezi ujao.

Mwenyekiti wa Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji ya TFF, Elias Mwanjala ndiye aliyefichua taarifa hizo katika mahojiano na Mwanaspoti.

Kauli ya Kamati hiyo ya TFF imekuja baada ya jana gazeti hili kuandika taarifa ya mabosi wa Jangwani kusema kwa sasa wameamua kuacha kumzungumzia mchezaji huyo ambaye amekuwa na matukio kadhaa ya utovu wa nidhamu kiasi cha kufikia kumlima faini ya Sh 1.5 milioni, kwa madai wanaliacha suala hilo kwa TFF wenyewe.

Mwanjala alisema, Morrison alifungua malalamiko kwao akidai kuwa saini yake katika mkataba mpya wa miaka miwili imeghushiwa na hivyo hautambui mkataba huo.

Mwenyekiti huyo alisema kutokana na suala hilo linahitaji uchunguzi wa vyombo vya dola na wao siyo wataalamu wa masuala la kughushi, wameamua kuwakabidhi na watoe majibu kabla ya kuanza kwa msimu mpya wa usajili wa wachezaji mwezi ujao.

“Siwezi kuingia ndani kuhusiana na suala hilo ambalo lipo katika uchunguzi, sipaswi kusema wapi, ila kama mwenyekiti, hali hiyo ndiyo ipo kwa sasa, tuache vyombo vya dola vifanye kazi yake,” alisema Mwanjala.

Kuhusiana na suala la fedha alizopewa Morrison kurejeshwa Yanga, Mwanjala alisema kuwa hakuna taarifa hiyo mpaka sasa zaidi ya kusubiri uchunguzi kukamilika.

“Ninachojua ni kwamba fedha ambazo Morrison alitaka kuzirudisha hazijarudi mpaka sasa, sina taarifa ya ndani kuhusiana na hilo. Naomba wadau wa soka kusubiri nini ambacho vyombo vya dola vitasema na sisi kutangaza uamuzi,” alisema.

Mbali ya Morrison kuishitaki Yanga, mabingwa hao wa kihistoria pia wameishitaki klabu ya Simba ikidai inaingilia mkataba wake na mchezaji huyo kinyume cha utaratibu, japo mabosi wa Msimbazi mara kadhaa wamekuwa wakikanusha tuhuma hizo.

Alisema, Yanga imewasilisha ushahidi wao kuhusiana na suala hilo ambapo Simba nao imeleta utetezi kuhusiana utetezi wake.

“Kwa kifupi masuala yote haya tutayatolea uamuzi kesho (leo) kwani kuna mengi sana, kuna suala la wachezaji kudai mishahara yao, masuala ya mikataba na kesi mbalimbali,” alisema.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Msaidizi wa Upelelezi Makosa ya Jinai nchini, Charles Kenyela alisema hawezi kuzungumzia suala hilo kwa sababu hakuwepo jijini Dar es Salaam kwani alikuwa Dodoma kikazi.

“Mimi sina taarifa ya suala hilo, labda Mkurugenzi Mkuu wa Makosa ya Jinai anaweza kuwa na taarifa rasmi, naomba mtafute akupe taarifa kama zipo,” alisema Kenyela kwa njia ya simu ingawa bosi wake alipotafutwa simu iliita bila majibu.